Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Yanga imekwama kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) baada ya kutupwa kwa rufaa yao iliyopinga kufutwa ghafla kwa mechi yao ya Ligi Kuu NBC dhidi ya mahasimu wao Simba.
Taarifa ya kutupwa kwa rufaa hiyo imepatikana leo Mei Mosi, 2025 kupitia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na tayari bodi hiyo imeahidi kupanga siku nyingine ya kuchezwa mechi hiyo.
Yanga na Simba zilipangwa kucheza Machi 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, mechi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki lakini ghafla mechi hiyo ilifutwa Machi 8 hiyo hiyo.
Uamuzi wa kuifuta mechi hiyo ulikuja baada ya kuibuka utata kutokana na kilichodaiwa kuwa Simba waliokuwa timu mgeni kuzuiwa kuutumia uwanja huo kwa mazoezi kama taratibu zinavyotaka.
TPLB kabla ya kuchukua uamuzi wa kuifuta mechi hiyo na kuahidi kuipangia siku nyingine, iliainisha matukio kadhaa yaliyohusiana na Simba kuzuiwa kuutumia uwanja huo ikiwamo taarifa ya ofisa usalama wa mchezo huo.
Kutokana na hali hiyo TPLB walitangaza kuahirisha mechi hiyo kwa madai kwamba matukio hayo yalihitaji uchunguzi ambao usingeweza kukamilika haraka na hivyo wakaona ni busara kuahirisha mchezo huo wa timu hizo mahasimu wa soka Tanzania.
Uamuzi huo uliwafanya Yanga kuwasilisha malalamiko yao CAS wakilishitaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo linashirikiana kwa karibu na TPLB katika usimamizi wa ligi na soka la Tanzania kwa ujumla.
Yanga katika madai yao CAS walitaka mechi hiyo isipangiwe siku nyingine na TPLB wakati wakisubiri uamuzi wa CAS.
Mshitakiwa mwingine katika sakata hilo ni Simba lakini kwa uamuzi huo wa CAS ni dhahiri kwamba mashabiki watapata nafasi ya kuziona timu hizo zikichuana siku nyingine itakayotangazwa na bodi hiyo.
Uamuzi huo wa CAS unakuwa umefuta mijadala ya baadhi ya mashabiki hasa wa Yanga ambao walikuwa wakitaka timu yao igomee mechi hiyo hali ambayo iliibua makundi baina yao wengine wakitaka mechi isigomewe na wengine wakisisitiza lazima igomewe.
Kimataifa Yanga yakwama CAS, rufaa yatupwa
Yanga yakwama CAS, rufaa yatupwa
Read also