Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Rodrygo, 24, inadaiwa yuko mbioni kuihama timu hiyo wakati wa dirisha kubwa la usajili la Majira ya Kiangazi baadaye mwaka huu huku Liverpool ikitajwa kumtaka.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari nchini Hispania, nyota huyo kutoka nchini Brazil inaaminika kuwa haioni nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Awali ilionekana kusajiliwa kwa Jude Bellingham kunamuweka pagumu mchezaji huyo lakini hali inadaiwa kuwa tete zaidi baada ya Real Madrid kumsajili Kylian Mbappe kutoka PSG.
Kutokana na hali hiyo Rodrygo ameamua ni bora msimu ujao atafute ustaarabu mwingine nje ya klabu hiyo maarufu duniani kwa kusajili wanasoka mastaa wa bei mbaya.
Na ingawa bado haijafahamika mara moja timu ambayo atapenda kujiunga nayo, kilicho wazi ni kwamba mbali na Liverpool iliyoonesha nia hiyo, klabu kadhaa kubwa barani Ulaya zitakuwa tayari kumchukua iwapo Real Madrid itamuacha aondoke.
Rodrygo alijiunga na Real Madrid mwaka 2019 akitokea Santos ya Brazil na kusaini mkataba unaoishia Juni 2025 lakini mwaka 2023 aliongeza miaka mitatu na hivyo mkataba huo sasa unafikia mwisho Juni 2028.
Liverpool inadaiwa ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumtaka Rodrygo kabla ya Real Madrid lakini haikufanikiwa kumpata na sasa haitokuwa ajabu kwa mchezaji huyo kujiunga na timu hiyo.
Kimataifa Rodrygo kuhama Real Madrid
Rodrygo kuhama Real Madrid
Read also
