Rio de Janeiro, Brazil
Shirikisho la Soka Brazil (CBF) limepanga kusubiri hatma ya Real Madrid katika mbio za kulisaka taji la La Liga itakapojulikana kabla ya kumuajiri kocha wa timu hiyo, Carlo Ancelotti.
Real Madrid kwa sasa ipo nyuma ya mahasimu wao Barcelona kwa tofauti ya pointi nne huku zikiwa zimebakia mechi tano kabla ya kumalizika ligi hiyo kwa msimu huu wa 2024-25 ambapo timu hizo zitakutana Mei 11.
Habari za ndani hata hivyo zinadai kwamba kilichobaki sasa ni makubaliano ya namna nzuri ya Real Madrid kuachana na Ancelotti kabla ya kocha huyo kukubali kibarua cha kuinoa timu ya Brazil.
Kwa sasa CBF wameamua iwe isiwe hadi Mei 26 mwaka huu lazima wawe wameajiri kocha mpya ambaye kikosi chake kitatangazwa wakati huo kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia 2026 zitakazopigwa mwezi ujao dhidi ya Ecuador na Paraguay.
Inadaiwa kukamilika kwa mpango huo kunasubiri kikao kati ya Ancelotti na rais wa Real Madrid, Florentino Perez, kikao ambacho kitafanyika hivi karibuni ili kuliweka sawa jambo hilo.
Ancelotti ambaye mkataba wake wa sasa na Real Madrid unafikia mwisho mwaka 2026, amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na CBF ili kuinoa timu hiyo kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2026.
Kwa mantiki hiyo suala la makubaliano ya kuvunja mkataba wa kocha huyo na Real Madrid huenda likawa na ugumu wake ingawa hapo hapo kuna ukweli kwamba Real Madrid nao hawana nia ya kuendelea na kocha huyo kutokana na matokeo yasiyopendeza ya timu hiyo msimu huu.
Iwapo Ancelotti ataamua kukimbilia kibarua cha kuinoa Brazil atajiweka katika nafasi kubwa ya kupoteza sehemu kubwa ya malipo hasa kwa kuwa Real Madrid nao wana nia ya kupiga pesa kupitia mkataba wa kocha huyo.
Real Madrid licha ya kwamba haina nia ya kuendelea na Ancelotti msimu ujao lakini inatambua kwamba CBF wanamtaka na kwao hiyo ni fursa ya kukaa mezani na kujadili namna ya kulipana.
Kimataifa Ancelotti kuinoa Brazil sasa ni suala la muda tu
Ancelotti kuinoa Brazil sasa ni suala la muda tu
Read also