Na mwandishi wetu
Simba imefuzu hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka sare ya 0-0 na Stellenbosch ya Afrika Kusini leo Jumapili Aprili, 27, 2025 kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Durban, Afrika Kusini.
Kwa matokeo hayo Simba inakuwa imefuzu kwa ushindi wa bao 1-0, ushindi ilioupata katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita bao hilo likifungwa na Jean Ahoua kwa mpira wa adhabu.
Stellenbosch licha ya kushindwa kupata bao leo lakini walionesha uhai na katika dakika ya 20, Chumani Butsaka aliishtua safu ya ulinzi ya Simba baada ya kufumua shuti ambalo lilitoka nje ya lango.
Zikiwa zimebakia dakika tano timu kwenda mapumziko mshambuliaji wa Stellenbosch, Andre de Jong alikosa umakini baada ya kuupiga mpira wa kichwa ambao ulitoka juu ya lango la Simba.
Dakika 10 baada ya timu kutoka mapumziko, Stellenbosch walijipa matumaini ya kupata penalti kwa madai kwamba beki mmoja wa Simba aliunawa mpira lakini maamuzi hayo yalifutwa baada ya mwamuzi kujiridhisha kwa kutumia VAR.
Stellenbosch waliendelea na makali yao na katika dakika ya 64 krosi iliyotokea upande wa kushoto wa Simba ilizaa bao lililofungwa na Palace aliyeingia kuchukua nafasi ya Butsaka.
Katika hali ambayo haikutarajiwa kwa mara nyingine tena bao lilikataliwa kwa kutumia VAR kwa kile kilichoonekana kuwa kuna mchezaji wa Stellenbosch aliyekuwa ameotea.

Baada ya kuona mambo yanakuwa magumu, Stellenbosh hasa katika dakika 10 za mwisho waliweka mkazo zaidi katika mashambulizi lakini umahiri wa safu ya ulinzi ya Simba hasa kipa Musa Camara ulikuwa kikwazo.
Camara mara kadhaa baada ya kuokoa mipira hiyo alitumia mbinu ya kuchelewesha muda kwa kujiangusha chini na mpira na wakati mwingine kulalamika kuumia na haikushangaza kwa mwamuzi kuongeza dakika nane baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika.
Simba nao mara kadhaa waliwaweka pagumu Stellenbosch mfano dakika ya 63, Kibu Dennis alionesha uwezo binafsi na kumzunguka beki kabla ya kupiga krosi lakini mpira ulikuwa wa juu kidogo na kumshinda Shomari Kapombe aliyekuwa karibu na lango.
Dakika 10 baadaye Elly Mpanzu aliwazunguka vyema mabeki wa Stellenbosh na kuambaa na mpira kabla ya kufumua shuti lakini kipa Oscarine Masuluke aliokoa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Katika kilichoonekana kuwa ni kuimarisha ulinzi baadaye kocha wa Simba Fadlu Davids aliwatoa Jean Ahoua na kumuingiza Debora Fernandes na baadaye akamtoa Mohamed Hussein Zimbwe Jr na kumuingiza Valentino Ouma na Mpanzu akatoka na kuingia Chemalone Fondoh.
Awali kabla ya mabadiliko hayo, Fadlu alimtoa Steven Mukwala na kumuingiza Lionel Ateba ambaye Simba ilianza kumpelekea mipira mingi upande wake.
Mabadiliko ya kuimarisha ulinzi kwa Simba bado hayakuizuia Stellenbosch kulisakama lango la Simba lakini safu ya ulinzi ya timu hiyo ilifanikiwa kudhibiti kila hatari iliyoelekezwa kwenye lango lao.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Simba kufikia hatua ya fainali ya michuano ya klabu inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) tangu kufanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1993.
Rais Samia awapongeza
Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Simba kwa kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, salamu alizozitoa muda mfupi baada ya dakika 90 kumalizika.
Katika salamu hizo zilizopatikana kwenye mitandao ya kijamii, Rais Samia aliipongeza Simba kwa kuandika historia ya kufikia hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Rais Samia katika salamu hizo pia alisema kwa hatua hiyo, Simba wameipa heshima nchi na kuwatakia kila la kheri huku akisisitiza kwamba wanayo hamasa yake wakati wote.
Simba sasa inasubiri kucheza mechi ya fainali na mshindi wa mechi kati ya RS Berkane na CS Constantine, mechi ambayo inachezwa jioni hii.