Madrid, Hispania
Baada ya Real Madrid kulala kwa mabao 3-2 mbele ya mahasimu wao Barcelona au Barca kwenye Kombe la Mfalme, ni wazi sasa kibarua cha kocha Carlo Ancelotti kipo njia panda.
Real Madrid imetolewa kwa fedheha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya robo fainali baada ya kulala kwa jumla ya mabao 5-1 mbele ya Arsenal.
Ilifungwa 3-0 ugenini Emirates lakini ikajipa matumaini kwamba inaweza na ina kila sababu ya kuitoa Arsenal katika mechi ya marudiano nyumbani, Santiago Bernabeu lakini nako ikafedheheshwa kwa kipigo cha mabao 2-1.
Kipigo hicho kilitosha kuanza kuzungumzwa kile kilichozungumzwa sana wiki kadhaa kabla kwamba mwisho wa Ancelotti katika kikosi cha Real Madrid umetimia.
Na hiyo ni kwa sababu mbio za timu hiyo kulisaka taji la Ligi Kuu Hispania au La Liga nazo ni ngumu, mahasimu wao Barca hawashikiki kileleni huku wakiendelea kutoa dozi.
Awali faraja pekee iliyobaki kwa Ancelotti ni Kombe la Mfalme au Copa del Rey lakini pia hali imekuwa tete jana Jumamosi mjini Sevilla baada ya kukumbana na kipigo mbele ya Barca.
Ancelotti atakwenda wapi?
Kwa sasa kinachozungumzwa kuhusu Ancelotti ni wapi atakuwa msimu ujao kwani kuondoka kwake Real Madrid kwa sasa ni suala la muda tu.
Heshima aliyoipata kwa kubeba mara mbili taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Real Madrid haitoshi kuwafanya vigogo wa klabu hiyo wambakishe badala yake wanamuona kama ameishiwa mbinu.
Ancelotti ambaye amekuwa na Real Madrid kwa vipindi viwili, kuanzia 2013 hadi 2015 na kurudi tena 2021 hadi sasa, mkataba wake unafikia ukomo 2026 lakini hakuna dalili zozote za klabu hiyo kuendelea kuwa naye kwa mwaka mwingine mmoja.
Amewahi kunukuliwa akisema kwamba lolote linawezekana na kwamba mazungumzo kuhusu mkataba wake yafanyika baada ya msimu huu huku kinachotarajiwa na wengi ni kwamba mazungumzo hayo yatakuwa ya kukubaliana kuachana na kocha huyo.
Kwa upande mwingine zipo habari kwamba Ancelotti anasakwa kwenye timu ya taifa ya Brazil kukiwa na matumaini kwamba anaweza kuwa mwarobaini wa matatizo yanayoikabili timu hiyo.
Brazil, taifa lenye heshima yake kwenye soka duniani kwa sasa mambo yake si mazuri, fukuza kufuza ya makocha imeendelea kupamba moto kama njia ya kusaka suluhisho lakini hali bado haijatulia huku jina la Ancelotti likizidi kuchomoza.
Zipo habari kwamba mazungumzo ya awali yameanza yakihusisha wawakilishi wa Ancelotti na vigogo wenye mamlaka ya usimamizi wa soka nchini Brazil.
Kimataifa Mwisho wa Ancelotti Real Madrid
Mwisho wa Ancelotti Real Madrid
Read also