Vatican City, Vatican
Mechi nne za ligi kuu ya soka ya Italia maarufu, Serie A zimeahirishwa kufuatia kifo cha Papa Francis ambaye amefariki leo Jumatatu Aprili 21 akiwa na umri wa miaka 88.
Taarifa ya kifo hicho imetangazwa rasmi na mamlaka za Vatican leo ikiwa ni siku kadhaa zimepita baada ya kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kutoka hospitali alikolazwa kwa takriban wiki tano.
Kifo hicho kimekuja ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi huyo kuonekana Jumapili ya Pasaka akiwa kwenye kiti cha magurudumu na kuwabariki waumini wa kikristo.
Mechi ambazo zimeahirishwa ni kati ya Torino dhidi ya Udinese, Cagliari na Fiorentina, Genoa na Lazio na Parma dhidi ya Juventus.
Bodi inayosimamia soka la Italia imetangaza uamuzi huo na kuahidi kuzipangia siku nyingine mechi hizo badala ya leo Jumatatu ambayo kwa kawaida ni siku mapumziko nchini Italia.
Papa Francis aliteuliwa kuongoza kanisa katoliki duniani mwaka 2013 akichukua nafasi ya Papa Benedict XVI aliyeushtua ulimwengu baada ya kuamua kung’atuka katika cheo hicho.
Kihistoria Papa Francis anatokea Argentina, alifahamika kwa kipindi kirefu kuwa mpenda soka na wakati akiwa kijana mdogo alikuwa shabiki wa timu ya San Lorenzo ya Argentina
Kutokana na msiba huo mkubwa klabu kadhaa za soka nchini Italia zimetuma salamu za rambirambi mojawapo ikiwa na klabu ya Roma ambayo imeeleza kuwa jiji lote la Roma na dunia kwa ujumla imesikitishwa na msiba huo.
“Imani yake, uvumilivu, ujasiri na kujitoa kwake ni mambo yaliyogusa mioyo ya mamilioni ya watu na kumfanya awe kielelezo cha kiroho katika zama zetu,” ilieleza taarifa ya klabu ya Roma.