Na mwandishi wetu
Simba imeanza vizuri mechi ya kwanza ya nusu fainali Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuilaza Stellenbosch ya Afrika Kusini bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, leo Jumapili, Aprili 20, 2025.
Bao pekee la Simba lilipatikana dakika ya 45 mfungaji akiwa ni Jean Ahoua kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja hadi wavuni na kumshinda kipa Oscarine Masuluke.
Bao hilo liliibua utata baada ya wachezaji wa Stellenbosch kugomea wakidai wachezaji wa Simba waliotea hivyo kulazimika kutumia VAR kabla ya kutangazwa kuwa ni bao halali.
Simba waliutawala vyema mchezo huo kwa wachezaji wake kuonesha ubora wao wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini tatizo la umaliziaji liliendelea kuiathiri timu hiyo.
Moja ya nafasi ya mapema Simba kuipata ni pale Kibu Dennis alipoambaa na mpira akiwa upande wa kushoto wa Stellenbosch na kupiga krosi ambayo Shomari Kapombe alibinuka vyema na kuupiga mpira staili ya tikitaka lakini mpira huo ulipaa nje ya lango.
Kasi ya Simba iliendelea na katika dakika ya 30, Ahoua aliunasa mpira na kumuunganishia Elly Mpanzu ambaye aliukokota kidogo kabla ya kufumua shuti kali la mguu wa kushoto ambalo liliokolewa vyema na kipa wa Stelenbosch.
Baada ya kuona kasi ya Simba inawazidi wachezaji wa Stellenbosch walianza kucheza rafu na mwamuzi kulazimika kuwapa kadi za njano Enyimnaya na Jabaar kwa kuwachezea rafu Mpanzu na Kibu.
Dakika tano baadaye Stellenbosch nao walijibu shambulizi baada ya kipa kuokoa mpira wa kona na kuwasaidia kutengeneza shambulizi lililoelekezwa upande wa kulia wa Simba.
Shambulizi hilo hata hivyo lilikwama baada ya Zimbwe Jr aliyehamia upande huo kumdhibiti mchezaji wa Stellenbosch wakati huo Kapombe anayecheza zaidi upande wa kulia akiwa amehamia upande wa kushoto ambao anacheza Zimbwe.
Kipindi cha pili, Stellenbosch walikianza kwa kufanya mabadiliko kadhaa yaliyoonekana kuwapa uhai na kumuweka katika wakati mgumu kipa Musa Camara wa Simba.
Simba nao walibadilika na kuanza kulisakama lango la wapinzani wao kwa kutengeneza nafasi nyingi ambazo hata hivyo walikwama katika kuzitumia nafasi hizo.
Nafasi mojawapo ya mwisho ni ile waliyoipata ikiwa imebaki dakika moja katika dakika sita za nyongeza baada ya Ahoua kuunganishiwa pasi ya chinichini na Mpanzu naye kumlamba chenga kipa Masuluke lakini shuti alilopiga la mguu wa kushoto lilitoka nje.
Katika mechi hiyo timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa, Stellenbosch wakiwatoa De Jong na kumuingiza Bans na Jabaar ambaye nafasi yake aliingia Palace.
Simba iliwatoa Zimbwe na kuingia Valentine Nouma, Kibu akaingia Joshua Mutale, Deborah Fernandes akaingia kuchukua nafasi ya Chamaou Karabou wakati Ateba akaingia kuchukua nafasi ya Steven Mukwala.
Timu hizo zinatarajia kurudiana Aprili 27 nchini Afrika Kusini, mechi ambayo mshindi atajikatia moja kwa moja tiketi ya kucheza mechi ya fainali ya michuano hiyo dhidi ya mshindi wa mechi ya nusu fainali nyingine kati ya CS Constantine na RS Berkane.