Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amekana kuwapo mgogoro wa chinichini katika klabu hiyo huku akiweka wazi kwamba mambo yake ya baadaye yatajadiliwa mwisho wa msimu huu.
Nafasi ya Ancelotti imekuwa mjadala katika siku za karibuni hasa baada ya timu hiyo kuishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutolewa na Arsenal.
Real Madrid ikiwa nyumbani Santiago Bernabéu Jumatano iliyopita ililala kwa mabao 2-1 mbele ya Arsenal hiyo ni badaa ya kulala ugenini kwa mabao 3-0 na hivyo kutolewa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 5-1.
Kocha huyo Mtaliano tangu ajiunge kwa mara ya pili na Real Madrid mwaka 2021 ameweza kujiwekea rekodi nzuri ya kubeba mataji ya La Liga mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili.
Msimu huu hata hivyo umekuwa mgumu kwa Ancelotti, timu yake imetolewa kwenye ligi ya mabingwa, michuano ambayo ina hadhi ya juu Ulaya na dunia kote wakati huo huo inahaha kubeba taji la La Liga.
Real Madrid msimu huu imepoteza mechi kadhaa katika namna ambayo haikutarajiwa, wiki ijayo itacheza mechi ya fainali Kombe la Mfalme, taji inalotakiwa ilipiganie walau itoke na kitu msimu huu.
“Nimezungumza na wachezaji na viongozi, sote tunafikiria katika mtazamo mmoja ambao ni kuendelea kupigania mataji yaliyobaki,” alisema Ancelotti.
Ancelotti alisisitiza kwamba hakuna mgogoro wowote na klabu na kwamba wote wapo katika safari moja na yeyote anayesema kuna mgogoro na klabu au rais (Florentino Perez) huyo hasemi ukweli.
Mkataba wa Ancelotti na Real Madrid unafikia ukomo mwaka 2026 ingawa kumekuwapo habari kwamba klabu hiyo inataka kuachana na kocha huyo ambaye pia inadaiwa anawindwa kwa udi na uvumba kwenye timu ya taifa ya Brazil.