Na mwandishi wetu
Kamati ya Maadili ya TFF imemtoza faini ya Sh milioni 5, meneja habari na mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe baada ya kumkuta na hatia katika kosa la kuchochea umma.
Maamuzi ya kamati hiyo ambayo yametangazwa leo Jumamosi, Aprili 19, 2025 kwenye taarifa ya TFF, pia yamemkosa na hatia meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ambaye kama Kamwe wote walikuwa na tuhuma za kuchochea umma.
Wakati Ahmed alishitakiwa na Yanga kwa kosa hilo, Kamwe yeye alishitakiwa na kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi na amepewa onyo na kutakiwa kutofanya kosa hilo kwa kipindi cha miaka miwili.
Taarifa ya TFF haijataja makosa hayo yalifanyika lini lakini inaaminika ni baada ya kuahirishwa mechi baina ya Yanga na Simba ambayo awali ilipangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu.
Baada ya mechi ya Yanga na Simba ambayo ni ya Ligi Kuu NBC kuahirishwa, yaliibuka malumbano baina ya viongozi wa timu hizo kwa kila upande kumtupia lawama mwenzake.
Mwingine aliyekutwa na hatia ya kosa la kuchochea umma ni ofisa habari wa Kagera Sugar, Hamis Mazanzala ambaye pia ametozwa faini ya Sh milioni tano.
Mwingine aliyekumbana na adhabu hiyo ni mwanachama wa klabu ya Simba, Mohamed Hamis Mohamed ambaye kama walivyo wenzake, wote wameanza kutumikia adhabu hizo Aprili 16 mwaka huu.
Wafungiwa maisha
Katika hatua nyingine kamati ya maadili ya TFF imemfungia maisha kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi, Shufaa Jumanne Nyamlani ambaye ni mtunza vifaa wa timu ya taifa ya Beach Soccer.
Shufaa ambaye pia alikuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama cha Soka Wilaya ya Temeke (Tefa) alishitakiwa na Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) kwa makosa matatu.
Makosa hayo ni kuchochea umma, kutoheshimu maamuzi ya vyombo halali vya usimamizi wa soka na kutaka kuiondoa madarakani kamati ya utendaji ya Tefa na licha ya kuitwa kwa ajili ya shauri lake lakini hakuitikia wito huo.
Mwingine aliyefungiwa maisha ni Salehe Mohamed Salehe aliyekuwa makamu mwenyekiti Tefa ambaye naye alikuwa akituhumiwa kwa makosa kama ya Shufaa lakini naye hakuitikia wito wa kwenda kusikiliza tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Soka Ally Kamwe atozwa faini milioni 5, wengine wafungiwa maisha
Ally Kamwe atozwa faini milioni 5, wengine wafungiwa maisha
Read also