New York, Marekani
Nyota wa mchezo wa tenisi wa Marekani, Serena Williams (pichani) amesema kama yeye angekutwa na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu angefungiwa miaka 20 na kunyang’anywa tuzo zote za Grand Slams alizobeba.
Serena alitoa kauli hiyo akionekana kushangazwa na adhabu aliyopewa bingwa namba moja wa mchezo huo duniani kwa upande wa wanaume, Jannik Sinner ambaye alikutwa na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu na Februari mwaka jana akafungiwa miezi mitatu.
Sinner alikubali kufungiwa miezi mitatu baada ya makubaliano na Wada, taasisi ya kimataifa inayojihusisha kukabiliana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu.
Wada walifikia hatua hiyo baada ya kupinga maamuzi ya tume huru iliyoamua kumfutia Sinner kosa hilo licha ya kupimwa mara mbili na kubainika kuwa alikuwa akitumia dawa hizo.
Serena alisema anampenda Sinner kwani ni shujaa katika mchezo wa tenisi na ingawa yeye amekuwa akishushwa chini sana lakini kwa upande wake hapendi kumshusha mtu hasa kwa kuwa mchezo wa tenisi kwa wanaume unamhitaji Sinner.
“Hata hivyo ukweli ni kwamba ningekuwa mimi ningefungiwa miaka 20 na kunyang’anywa tuzo zangu zote za Grand Slams,” alisema Serena ambaye amewahi kushinda Grand Slams kwa mara 23.
Serena, 43, alisema kwamba wakati wote katika mchezo wa tenisi amekuwa makini kwa kila kitu anachokiingiza mwilini mwake kwa hofu ya kuingia kwenye matatizo.
Katika hali ya dhihaka, Serena alisema kwamba jambo dogo tu lingeweza hata kumpeleka jela na kusikika kila kona katika namna nyingine.