Na mwandishi wetu
Simba imefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho CRDB kwa kuilaza Mbeya City mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa Jumapili hii Aprili 13, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Mbeya City ndio walioanza kwa kuwashtua Simba baada ya kuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 22 lililofungwa na Mudathir Abdullah ambaye aliitumia pasi ndefu ya William Daniel.
Baada ya kuinasa pasi hiyo, Abdullah aliwazidi ujanja mabeki wa Simba, Abdulrazak Hamza na Chamou Karabou kabla ya kufumua shuti la mguu wa kushoto lililomshinda kipa Ally Salim na kujaa wavuni.
Simba walionesha utulivu na dakika tatu baadaye walisawazisha bao hilo mfungaji akiwa Fabrice Ngoma ambaye aliinasa krosi ya Ladack Chasambi na kuunganisha mpira huo kwa kichwa hadi wavuni.
Kasi ya Simba iliendelea kuwaweka pagumu Mbeya City ambao walijikuta wakichapwa bao la pili mfungaji akiwa ni Leonel Ateba akiitumia krosi ya Ngoma.
Zikiwa zimebaki dakika mbili timu kwenda mapumziko, Simba waliandika bao la tatu lililofungwa na Joshue Mutale ambaye alionesha juhudi binafsi hadi kufunga bao hilo.
Mutale akiwa na mpira aliwazidi ujanja mabeki kadha wa Mbeya City kabla ya kufumua shuti lililomzidi ujanja kipa wa Mbeya City, Hashim Mussa.
Baada ya mabao hayo Simba waliendelea kutawala mchezo kwa kulisakama lango la Mbeya City na kumuweka katika wakati mgumu kipa Hashim Mussa ambaye alifanya juhudi kuokoa michomo kadhaa ya wachezaji wa Simba.
Simba baada ya ushindi huo wa robo fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Benki ya CRDB, sasa inasubiri kucheza mechi ya nusu fainali na mshindi wa mechi kati ya Singida Black Stars na Kagera Sugar.
Soka Simba yatua nusu fainali Kombe la Shirikisho CRDB
Simba yatua nusu fainali Kombe la Shirikisho CRDB
Read also