Na mwandishi wetu
Hatimaye Yanga leo Jumatano Aprili 2, 2025 imebeba pointi tatu muhimu katika Ligi Kuu NBC baada ya kuilaza Tabora United mabao 3-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Kwa matokeo hayo Yanga imejiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 23 ikifuatiwa na mahasimu wao Simba wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 22.
Yanga ilianza kuandika bao la kwanza dakika ya 16 mfungaji akiwa ni beki Israel Mwenda kwa mpira wa adhabu iliyotolewa baada ya beki wa Tabora, Banele Junior kumchezea rafu Prince Dube.
Tabora wakishangiliwa na mashabiki wao wa nyumbani walipambana kutaka kusawazisha huku Hiritier Makambo akionekana kuisumbua safu ya ulinzi ya Yanga ingawa hadi muda wa mapumziko unafika walikuwa ni Yanga waliotoka uwanjani na bao hilo pekee.
Kipindi cha pili kila timu iliendelea kuonesha nia ya kutaka bao lakini alikuwa ni Clement Mzize aliyewainua vitini mashabiki wa Yanga dakika 10 baada ya mapumziko akiitumia pasi ya Pacome Zouzoua.
Yanga walikamilisha karamu ya mabao dakika ya 67 kwa bao la Dube ambaye aliinasa pasi ya Pacome na kumzunguka beki wa Tabora kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Jan Noel.
Dalili za ushindi kwa Yanga zilianza kuonekana mapema dakika ya 11 baada ya Ibrahim Bacca kuunganisha kwa kichwa kona iliyochongwa na Pacome lakini mpira aliopiga uligonga mwamba.
Dakika tatu kabla ya shambulizi hilo, Mzize naye alimpora mpira beki wa Tabora na kugongeana vyema na wachezaji wenzake na mpira kumrudia kabla ya kufumua shuti ambalo lilipaa juu ya lango.
Ushindi wa leo umepokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa Yanga baada ya majibizano na majigambo yaliyotawala kabla ya mechi hiyo lakini zaidi ikikumbukwa Yanga ilivyolala kwa mabao 3-1 timu hizo zilipokutana Novemba mwaka jana.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho Alhamisi kwa mechi kati ya JKT Tanzania na Dodoma Jiji, Kagera Sugar na Coastal Union na Ken Gold dhidi ya Azam FC.
Soka Tabora yachezea kichapo kwa Yanga
Tabora yachezea kichapo kwa Yanga
Read also