Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ameiambia mahakama moja nchini Hispania leo Jumatano Aprili 2, 2025 kwamba hakuwahi hata kufikiria kufanya kosa la ukwepaji kodi.
Ancelotti anatuhumiwa kukwepa kodi inayofikia Dola 1.08 milioni, kodi inayotokana na haki za matangazo ya picha kwa mwaka 2014 na 2015 alipokuwa kocha wa Real Madrid kwa mara ya kwanza.
“Kwangu mimi kila kitu kilikuwa katika utaratibu, sikuwahi hata kufikiria kukwepa kodi,” alisema Ancelotti baada ya kufika mahakamani hapo kwa mara ya kwanza.
Kocha huyo mkongwe aliwasili mahakamani akiwa na mtoto wake wa kiume, mmoja wa wasaidizi wake pamoja na rafiki yake wa kike na alitumia dakika zipatazo 40 kujitetea.
Ancelotti alisema alipojiunga na Real Madrid Julai 2013 alipewa mshahara wa Euro milioni sita na klabu ilitoa mgawanyo wa mshahara huo na yeye akafikisha taarifa hizo kwa mshauri wake wa masuala ya kodi aliyekuwa Uingereza.
“Sikuwa mwenye kulipa umuhimu wowote suala la haki za picha, makocha hawana umuhimu katika hilo, ni wachezaji ndio wenye umuhimu nalo, nilichokiangalia ni kujiingizia malipo ya Euro milioni sita katika kipindi cha miaka mitatu,” alisema Ancelotti.
Ancelotti alifafanua kuwa hakuwahi kujua kwamba kuna kitu ambacho hakikuwa sawa na hakuarifiwa kwamba alikuwa anachunguzwa.
Katika shauri hilo waendesha mashtaka wanataka mtuhumiwa huyo afungwe jela miaka minne na miezi tisa pamoja na kutozwa faini ya Euro milioni 3.2.
Madai ya waendesha mashtaka hao ni kwamba kwa mwaka 2014 hadi 2015, Ancelotti anadaiwa kutoa taarifa kwenye ofisi za kodi kuhusu mshahara pekee aliokuwa akilipwa na klabu hiyo na kuweka kando haki za picha.
Kocha ambaye alirudi tena kuinoa Real Madrid mwaka 2021 na kuendelea na kibarua hicho hadi sasa, anaingia katika orodha ya makocha na wachezaji mastaa wanaochunguzwa nchini Hispania kwa makosa ya ukwepaji kodi.
Wengine ni Cristiano Ronaldo na Diego Costa ambao kesi zao zilimalizwa nje ya mahakama na kutakiwa kulipa faini kubwa, pia yumo kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso ambaye alikataa kumaliza suala lake nje ya mahakama.
