Ismailia, Misri
Mambo si mazuri kwa Simba nchini Misri baada ya kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Al Masry katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa leo Jumatano, Aprili 2, 2025.
Simba iliyokuwa ugenini licha ya kulisakama lango la Al Masry kwa mashambulizi ya mara kwa mara lakini walishindwa kutumia nafasi nyngi walizotengeneza na hatimaye kupoteza mechi hiyo.
Kwa matokeo hayo Simba sasa itakuwa na kazi ngumu ya kufanya Aprili 9 timu hizo zitakaporudiana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mambo yalianza kuwaribikia Simba dakika ya 16 ya mchezo huo baada ya wenyeji Al Masry kuandika bao la kwanza lililofungwa na Abdelrahim Degmoum kwa shuti kali la mguu wa kushoto.
Shuti hilo la chinichini awali ilionekana kama kipa wa Simba Musa Camara angeudaka mpira huo lakini ulidunda na kumpoteza kabla ya kujaa wavuni.
Baada ya bao hilo Simba walionesha dhamira ya kutaka kusawazisha na dakika kama tano za mwisho kabla ya mapumziko, Al Masry walikuwa na kazi ya kuokoa na kujaribu kuchelewesha muda kwa namna ambavyo Simba waliwaweka katika wakati mgumu.
Tatizo la umaliziaji hata hivyo liliigharimu Simba kuanzia dakika ya 46 baada ya Kibu Denis kupora mpira na kuonesha uwezo binafsi lakini akiwa katika nafasi ambayo ilitarajiwa angetoa pasi alifumua shuti lililotoka nje.
Dakika tano baadaye, Elly Mpanzu alichezewa rafu na Tahir Taim na mwamuzi kuamuru upigwe mpira wa adhabu lakini shuti alilopiga Jean Ahoua liliokolewa na kipa wa Al Masry.
Simba walifanya shambulizi lingine dakika ya 70 baada ya Shomary Kapombe kutoa pasi ya kichwa kwa Ateba ambaye wakati akielekea kwenye lango la AL Masry kipa alimzuia kwa mkono na hatimaye mpira kutoka nje.
Tukio hilo liliwaamsha wachezaji wa Simba ambao waliamini mwamuzi angetoa penalti lakini hakufanya hivyo licha ya Ateba kulala chini akilalamikia kuumia na alichofanya mwamuzi ni kusimamisha mchezo.
Dakika ya 82 Kapombe alimuunganishia pasi Mpanzu ambaye licha ya kumtoka kipa lakini shuti alilopiga lilipaa juu ya lango na kuwaachia mshangao mashabiki wake.
Katika dakika ya 85 Steven Mukwala aliyeingia kuchukua nafasi ya Ateba alipiga krosi iliyompita Kibu na kutua miguuni mwa Kapombe lakini mchezaji huyo alishindwa kuumiliki vyema mpira miguuni na hatimaye mpira huo kutua mikononi mwa kipa wa Al Masry.
Wakati wote huo Al Masry walikuwa wakijihami na kusogea na mpira mara chache mno kwenye lango la Simba kabla ya kuwashtukiza kwa bao la dakika ya 89 lililotokana na juhudi za wachezaji walioingia kipindi cha pili ambao ni John Okoye aliyefunga akiitumia krosi ya Mohammed Hussein (si wa Simba).
Kimataifa Al Masry yailaza Simba 2-0
Al Masry yailaza Simba 2-0
Read also