Oujda, Morocco
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeshindwa kutamba mbele ya Morocco baada ya kulala kwa mabao 2-0 katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliyopigwa usiku wa kuamkia Jumatano ya Machi 26, 2025.
Wenyeji Morocco walipata mabao yao yote kipindi cha pili, la kwanza likifungwa dakika ya 51 na Nayef Aguerd, beki anayecheza Ligi Kuu Hispania au La Liga katika klabu ya Real Sociedad.
Dakika nane baadaye Stars ilichapwa bao la pili safari hii likifungwa kwa penalti mfungaji akiwa ni Ibrahima Diaz, kiungo ambaye pia anacheza soka Hispania na klabu ya Real Madrid.
Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya beki wa kati wa Stars, Ibrahim Bacca ambaye pia anaichezea Yanga kuunawa mpira ndani ya eneo la penalti.
Kwa matokeo hayo, Morocco sasa wanashika usukani wa Kundi E wakiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tano wakati Stars inashika nafasi ya tatu na pointi zake sita.
Niger inashika nafasi ya pili ingawa ina pointi sawa na Stars lakini ikineemeka kwa mabao wakati Zambia inashika mkia ikiwa na pointi tatu katika mechi nne.
Timu nyingine katika kundi hilo ni Jamhuri ya Congo au Congo Brazaville ambayo imefungiwa na Fifa wakati Eritrea imejitoa katika mashindano hayo.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinatarajiwa kufanyika katika nchi tatu za Marekani, Canada na Mexico.
Kimataifa Morocco yaipopoa Stars 2-0
Morocco yaipopoa Stars 2-0
Read also