Basel, Switzerland
Mahakama ya Rufaa ya Switzerlamd imewafutia mashtaka ya rushwa vigogo wa zamani wa soka duniani, Sepp Blatter ambaye alikuwa rais wa Fifa na Michel Platini aliyekuwa rais wa Uefa.
Uamuzi huo umefikiwa Jumanne hii, Machi 25, 2025 ikiwa ni zaidi ya miaka miwili imepita tangu wafutiwe mashtaka hayo kwa mara ya kwanza.
Blatter na Platini walikuwa na hadhi ya juu katika soka duniani wamefutiwa mashtaka ya rushwa katika Mahakama ya Juu ya Rufaa za Jinai
Uamuzi wa kusikiliza rufaa hiyo ulikuja baada ya wawili hao kufutiwa mashtaka ya rushwa mwaka 2022 lakini waendesha mashtaka wa Switzerland hawakukubaliana na uamuzi huo na kukata rufaa katika mahakama ya juu.
Blatter na Platini ambaye amewahi kuwa mwanasoka wa kimataifa aliyetamba na klabu kadhaa na timu ya taifa ya Ufaransa aliyokuwa nahodha wake, kwa wakati wote wamekuwa wakisisitiza kutofanya kosa lolote.
Kesi ya wawili hao imetokana na tuhuma za malipo ya Dola 2.25 milioni fedha ambazo inadaiwa mwaka 2011, Blatter aliidhinisha alipwe Platini.
Malipo hayo inadaiwa yalilipwa kwa ajili ya ushauri, kazi aliyoifanya Platini kati ya mwaka 1998 hadi 2002 lakini alidai kwamba alilipwa kwa mafungu kwa sababu Fifa haikuwa na fedha za kulipa zote kwa mkupuo mmoja.
Kashfa hiyo iliibuka mwaka 2015 na kuitikisa dunia ya soka wakati Platini akiwa rais wa Uefa akidaiwa kuwa na matarajio makubwa ya kumrithi Blatter katika kiti cha urais wa Fifa.
Mpango huo wa Platini hata hivyo haukufanikiwa na mwisho wa siku wawili hao wote walipoteza nafasi zao wakati wa kashfa hiyo.
Haijaweza kufahamika mara moja kama dhamira ya Platini mwenye umri wa miaka 69 kuwania nafasi ya urais wa Fifa bado ipo wakati kwa Blatter ni wazi umri wake wa miaka 89 ni mkubwa mno kwake kuwania nafasi hiyo.
Kimataifa Blatter, Platini wasafishwa kashfa ya rushwa
Blatter, Platini wasafishwa kashfa ya rushwa
Read also