Na mwandishi wetu
Simba imeilaza Dodoma Jiji 6-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC ilyopigwa leo Ijumaa Machi 14, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam huku Kibu Denis akifunga mabao mawili kati ya hayo na kuwa kama amefuta ukame wa mabao.

Kibu ambaye pia ameibuka mchezaji bora wa mechi hiyo, amekuwa na mchango mkubwa katika mabao ya timu hiyo kwenye ligi msimu huu lakini ni mara ya kwanza kuifungia Simba tangu afanye hivyo takriban mwaka mmoja na miezi minne iliyopita.
Mashabiki wa Simba wanakumbuka mara ya mwisho Kibu kuifungia bao timu yao ilikuwa kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao Yanga, mechi ambayo Simba ililala kwa mabao 5-1 huku bao pekee la Simba likifungwa na Kibu.
Baada ya kufunga bao la kwanza hii leo, Kibu alishangilia huku akionesha kama ishara ya kujifuta na kuanza upya akiwa kama anawaambia mashabiki hao kwamba sasa wataona makali yake kwani amefuta ukame uliokuwa ukimuandama.
Kwa ushindi huo Simba sasa imefikisha pointi 57 katika mechi 22 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga wanaoshika usukani wakiwa na pointi 58 katika mechi 22 kama za Simba.
Ushindi wa mechi ya leo ambayo ni ya kiporo ulianzia dakika ya 16 kwa bao la Elly Mpanzu ambaye aliizidi ujanja safu ya ulinzi ya Dom Jiji baada ya kuinasa pasi ya Kibu na kufumua shuti lililojaa wavuni.
Simba waliongeza bao la pili dakika ya 21 lililofungwa na Jean Ahoua ambaye aliitumia pasi ya chinichini ya Mohamed Hussein kabla ya kuupiga mpira uliogonga mwamba na kumshinda kipa Allain Ngereka.
Dom Jiji walipachikwa bao la tatu dakika ya 45 lililofungwa tena na Ahoua na kwa mara nyingine pasi ya Kibu ndiyo iliyozaa bao hilo.
Mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Dom Jiji kwani dakika moja tu baada ya kuanza kipindi cha pili, walipachikwa bao la nne mfungaji akiwa Steven Mukwala kwa kisigino akimalizia kazi nzuri ya Mpanzu.
Kibu aliwainua kwa mara nyingine vitini mashabiki wa Simba katika dakika ya 54 akifunga bao la kichwa kwa mpira wa kona ambapo alishangilia bao hilo kwa kuonesha ishara ya kujisafisha na ukame wa mabao uliokuwa ukimuandama.
Mashabiki wa Simba waliinuliwa tena vitini na Kibu ambaye aliifungia timu hiyo bao la sita na la mwisho katika dakika ya 65.
Simba pamoja na mabao hayo bado waliendelea kulisakama lango la Dom Jiji na dakika ya 88 bado kidogo wapate bao la saba kupitia kwa Ahoua lakini uimara wa kipa Ngereka ulikuwa kikwazo baada ya kuokoa shuti la Ahoua alilopiga chinichini.
