New York, Marekani
Rais wa Fifa, Gianni Infantino amekutana na Rais wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya Marekani na kuzungumzia mipango ya fainali za Kombe la Dunia 2026 huku Trump akihoji kama Marekani itabeba taji la michuano hiyo.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ijumaa hii kwenye Ikulu ya White House, Trump inadaiwa alimuuliza Infantino kama Marekani itaweza kushinda Kombe la Dunia na Infantino akaonesha kuwa jambo hilo linawezekana.
Sambamba na fainali za Kombe la Dunia 2026, Marekani itakuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia kwa Klabu ambazo zitafanyika baadaye mwaka huu.
Awali baada ya Trump kumuuliza Infantino nchi ambazo zinaweza kushinda Kombe la Dunia, Infantino akazitaJa na ndipo Trump alipomuuliza kuhusu Marekani ambayo haikuwa kwenye orodha ya awali ya Infantino.
“Brazil, Argentina, England, Hispania, Ujerumani,” alizitaja Infantino na ndipo Trump alipohoji iwapo Marekani inaweza kuishangaza dunia na kubeba taji hilo.
Katika ufafanuzi wa hoja hiyo, Infantino alimwambia rais huyo wa 47 wa Marekani kwamba nchi yake inaweza kubeba taji hilo kwa msaada wa mashabiki na hata timu yao ni moja ya timu bora duniani.
“Kwa hiyo uwezekano upo?” Alihoji zaidi Trump na Infantino akamjibu hapo hapo, “Hakika nafasi hiyo ipo.”
Trump pia alimuahidi Infantino kwamba ataunda kikosi kazi kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo safari hii zinafanyika Marekani ya Kusini kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994.
Marekani itakuwa mwenyeji wa fainali hizo ikishirikiana na nchi za Canada na Mexico ingawa nchi hizo kwa sasa zipo katika mzozo unaohusisha mambo ya kodi baada ya Trump kutaka bidhaa za nchi hizo majirani zake zitozwe kodi.
Trump hata hivyo anaamini mzozo wa mataifa hayo kuhusu masuala ya kodi utazifanya fainali hizo ziwe na hamasa zaidi.
Katika historia ya fainali za Kombe la Dunia, Marekani ina rekodi ya kufikia hatua ya nusu fainali mwaka 1930 katika fainali za kwanza katika historia ya michuano hiyo na baada ya hapo Marekani pia ilifikia hatua ya robo fainali mwaka 2002.
Kimataifa Trump ahoji nafasi ya Marekani kubeba Kombe la Dunia
Trump ahoji nafasi ya Marekani kubeba Kombe la Dunia
Read also
