Madrid, Hispania
Ofisi ya waendesha mashtaka wa Hispania imetaka kesi ya rais wa zamani wa shirikisho la soka Hispania, Luis Rubiale ya kumbusu mdomoni mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania, Jenni Hermoso isikilizwe upya.
Rubiales aliadhibiwa kwa kosa la udhalilishaji kijinsia na kutozwa faini ya dola 10,500 katika kesi ambayo ilikuwa mjadala mkubwa nchini Hispania na duniani kwa ujumla.
Katika kesi hiyo, Rubiales alishitakiwa kwa kumpiga Jenni busu la mdomoni bila ridhaa yake tukio lililotokea mwaka 2023 mjini Sydney, Australia wakati wa utoaji medali kwa wachezaji wa timu ya Hispania iliyobeba Kombe la Dunia kwa wanawake.
Uamuzi wa mahakama mbali na kumtoza faini Rubiales lakini uliwaachia huru watu wengine watatu waliodaiwa kuwa washirika wa Rubiales ambao pia walidaiwa kutetea na kumshawishi Jenni aseme kwamba alipigwa busu kwa ridhaa yake.
Awali waendesha mashtaka walitaka Rubiales afungwe jela miaka miwili na nusu lakini baada ya adhabu ya faini kutolewa, sasa wamewasilisha rufaa wakitaka kesi isikilizwe upya kwa madai kwamba ushahidi na maswali yao mengi havikufanyiwa kazi.
Katika hoja yao, ofisi ya waendesha mashtaka imedai kwamba faini aliyotozwa Rubiales na fidia ya Euro 3000 alizopewa Jenni vyote ni vya kiwango cha chini mno.
Tukio la busu hilo lilimuweka pagumu Rubiales ambaye pia alifungiwa na Fifa kujihusisha na soka kwa miaka mitatu na ingawa alikata rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Michezo lakini aligonga mwamba.
Rubiales pia alijikuta akishinikizwa kujiuzulu nafasi ya urais katika Shirikisho la Soka Hispania, awali alikataa akidai hana kosa lakini baadaye alikubali baada ya kusakamwa kila kona.
Pamoja na yote, Rubiales ameendelea kusisitiza kwamba kulikuwa na makubaliano kati yake na Jenni kabla ya kumpiga busu hilo lililozua taharuki.
Kimataifa Wataka kesi ya aliyembusu mchezaji mdomoni isikilizwe upya
Wataka kesi ya aliyembusu mchezaji mdomoni isikilizwe upya
Read also