Na Hassan Kingu
Mechi ya Ligi Kuu NBC baina ya mahasimu wa soka nchini Tanzania, Yanga na Simba iliyokuwa ichezwe leo Jumamosi Machi 8, 2025, imeahirishwa.
Uamuzi huo umetangazwa leo Jumamosi Machi 8 na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na taarifa zake kutufikia saa takriban nne kabla ya muda wa kuchezwa mechi hiyo.
Mechi ilipangwa kuchezwa majira ya saa moja na robo usiku kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam na uamuzi huo umefikiwa baadhi ya mashabiki wakiwa tayari wamefika uwanjani hapo.
Uamuzi wa bodi hiyo umekuja baada ya kuibuka sintofahamu kutokana na kitendo cha Simba ambao ni timu mgeni kuzuiwa na timu mwenyeji ambao ni Yanga kuutumia uwanja husika kwa ajili ya mazoezi kama taratibu zinavyotaka.
Simba baada ya kuzuiwa kufanya mazoezi iliwasilisha malalamiko yake TPLB huku ikielezea nia yake ya kutoshiriki mechi hiyo baada ya kunyimwa haki yao ya kikanuni ya kuutumia uwanja huo kwa ajili ya mazoezi.
Bodi kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB iliitisha kikao cha dharura na baada ya taarifa mbalimbali kuwafikia kutoka kwa maofisa wake na vyanzo husika ilibaini mambo kadhaa.
Kamati hiyo ilibaini kuwa Simba wakati wakielekea uwanjani kuitumia haki yao ya kuutumia uwanja huo kwa mazoezi haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo.

Simba pia haikuwasiliana na timu mwenyeji wala mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kuutumia uwanja huo kwa mazoezi ili maandalizi yafanyike kikanuni.
Kamati pia ilibaini kuwa walinzi ambao baadhi yao walifahamika kwa sura kuwa ni wa Yanga walishiriki tukio la kuzuia basi la Simba kuingia uwanjani kinyume na taratibu za mchezo wa ligi kuu.
Bodi pia ilipokea taarifa ya ofisa usalama wa mchezo ambayo imeainisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio la Simba kuzuiwa kufanya mazoezi.
Kutokana na matukio yote hayo bodi imeona yanahitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati na hivyo imeamua kuiahirisha mechi hiyo.
“Kutokana na matukio hayo bodi, kupitia kamati ya uendeshaji imeamua kuahirisha mchezo husika ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki,” ilieleza kwa ufafanuzi sehemu ya taarifa ya bodi.
Bodi pia imeahidi kutoa taarifa kamili kuhusu tukio hilo na kutangaza tarehe ya mchezo huo mapema iwezekanavyo.
Pigo kwa Yanga, mashabiki
Uamuzi wa kuahirisha mechi hiyo utakuwa pigo kubwa kwa mashabiki ambao baadhi yao wamesafiri kutoka mikoani na hata nje ya nchi kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo.
Mashabiki hao bila shaka wengi wao waliamini kuwa mechi inapochezwa Jumamosi, wnaaweza kuwa na muda wa kutosha kurejea mikoani kuendelea na shughuli zao kama kawaida kuanzia Jumatatu.
Kwa upande wa Yanga pia haijulikani hali itakuwaje kutokana na uamuzi huo kwani walishaahidi mapema katika taarifa yao kwamba hawatokuwa tayari kucheza mechi siku nyingine zaidi ya leo.
Je wataafikiana na uamuzi wa bodi kuahirisha mechi au watasimamia msimamo wao wa kutokuwa tayari kucheza mechi hiyo siku nyingine zaidi ya leo?