Barcelona, Hispania
Mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Barcelona, Deco amefuta uwezekano wa klabu hiyo kumsajili kwa mara nyingine mshambuliaji wa Brazil, Neymar Jr katika timu hiyo.
Neymar, 33, Januari mwaka huu aliamua kurudi katika klabu yake ya zamani ya Santos ya Brazil kwa mkataba wa muda mfupi baada ya makubaliano na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia aliyokuwa akiichezea.
Awali zilikuwapo habari kwamba hatua hiyo ya Neymar kuondoka Saudi Arabia malengo yalikuwa ni kurudi Ulaya huku Barcelona au Barca ikitajwa kuwa moja ya klabu ambayo ingemsajili.
Neymar aliwahi kuichezea Barca kabla ya kujiunga na PSG ya Ufaransa mwaka 2017 kwa usajili ulioweka rekodi ya Euro milioni 220 na baada ya hapo akatimkia Saudi Arabia katika klabu ya Al Hilal.
“Neymar ni mchezaji wa mfano na jambo la msingi kwa sasa ni kwamba ana furaha, kuwa kwake Brazil kunamfanya awe mwenye furaha na hilo ndilo analolifikiria na si suala la fedha,” alisema Deco.
Deco ambaye pia amewahi kuichezea Barca alisema kama kuna mambo ya baadaye kwa Neymar na Barca suala hilo litakuwa la Barca zaidi na yeye kwa kuwa timu za soka zinajengwa na vichwa tulivu na mazingira ya uwiano.
Alisema kwamba Neymar ni mchezaji wa mfano ambaye kuna mambo aliyafanya katika klabu ya Barca na kuna aliyoyashinda lakini kuna wakati ambao habari hizi hazijirudii.
“Huu si wakati wa Barcelona kumfikiria Neymar au yeye kufikiria kurudi hapa, kwa sasa yuko katika klabu yake ya Santos na ni sehemu sahihi kwake,” alisema Deco.
Mapema wiki hii kocha wa Barca, Hansi Flick alisema kwamba si kazi yake kufanya uamuzi wa kumsajili Neymar, ameliacha suala hilo mikononi mwa Deco.