Na mwandishi wetu
Yanga imekamata usukani wa Ligi Kuu NBC kwa kishindo baada ya kuigaragaza KMC mabao 6-1 huku kiungo Stephane Aziz Ki akifunga mabao matatu (hat trick) peke yake.
Ushindi huo uliopatikana Ijumaa hii, Februari 14, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam unaifanya Yanga kujikita kileleni mwa ligi hiyo kwa fikisha pointi 49.
Yanga imekusanya idadi hiyo ya pointi katika mechi 19 na kuwazidi mahasimu wao Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi mbili ingawa Yanga imecheza mechi 19 na Simba 18.
Karamu ya mabao ya Yanga katika mechi hiyo ilianza kuandikwa katika dakika ya 11 kwa bao la Prince Dube akiiitumia vizuri pasi ya Maxi Nzengeli.
Dakika saba baadaye, KMC waliumizwa kwa mara nyingine baada ya Aziz Ki kuifungia Yanga bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya Clement Mzize kuangushwa ndani ya eneo la 18.
Hadi timu zinakwenda mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao mawili na muda mchache baada ya kuanza kipindi cha pili, Aziz Ki ambaye pia aliibuka mchezaji bora wa mechi hiyo aliiongezea Yanga bao la tatu kwa shuti kali.
Mabao matatu ya Yanga hayakuwafanya KMC kukata tamaa ambapo dakika ya 52 walipata bao mfungaji akiwa ni Remdatus Mussa aliyefumua shuti lililomshinda kipa, Djigui Diarra.
Mambo hata hivyo yaliwaharibikia tena KMC dakika sita baadaye kwa Yanga kupata bao la nne lililofungwa tena kwa penalti na Aziz Ki, penalti iliyotolewa baada ya Dube kuangushwa ndani ya eneo la 18.
Yanga waliendelea kutawala mchezo na kuwanyanyasa wenyeji KMC kwa kuandika mabao mengine mawili yaliyofungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 90 na Israel Mwenda katika dakika tano za nyongeza.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Ken Gold na Tabora United zilitoka sare ya bao 1-1, Tanzania Prisons ililala kwa bao 1-0 mbele ya Namungo na Kagera Sugar iliilaza Fountain Gate 3-0.
Soka Yanga yaigaragaza KMC 6-1
Yanga yaigaragaza KMC 6-1
Read also