Na mwandishi wetu
Matarajio ya Simba kuiengua Yanga kileleni kwa msimamo wa Ligi Kuu NBC yamekwama leo Alhamisi, Februari 6, 2025 baada ya timu hiyo kutoka sare ya bao 1-1 na Fountain Gate FC.
Simba ikiwa ugenini Manyara kwenye Uwanja wa Kwaraa imeshindwa kufanya kilichotarajiwa na mashabiki wake na kuambulia pointi moja inayowafanya wabaki nafasi ya pili.
Mashabiki wa Simba walikuwa na matarajio makubwa kwa timu yao kupata ushindi mwingine wa kuwapa pointi tatu ambazo zingewatoa Yanga kileleni kwa kuwazidi kwa pointi moja.
Matokeo hata hivyo yamekuwa tofauti na Simba inabaki nafasi ya pili na pointi 44 wakati mahasimu wao Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo wakijinafasi kileleni na pointi zao 45.
Simba walipambana kusaka bao la mapema lakini ukuta wa Fountain Gate ulikuwa mgumu na haikushangaza kwa timu hiyo kupata bao lao katika dakika ya 57, mfungaji akiwa Leonel Ateba kwa pasi ya Ladack Chasambi.
Bao hilo lilianzia kwa mpira wa adhabu uliopigwa kwa haraka na Jean Ahoua na kumkuta Chasambi aliyetoa pasi ya bao jambo ambalo liliwakera wachezaji wa Ken Gold ambao walimlaumu mwamuzi Abel William wakionekana kutoridhishwa kwa namna Ahoua alivyopiga mpira kwa haraka.
Mambo hata hivyo yaliwaharibikia Simba baada ya Chasambi aliyetoa pasi ya bao kujifunga dakika ya 76 wakati akimpa pasi ya nyuma kipa wake Musa Camara lakini akakosea hesabu na mpira kujaa wavuni.
Juhudi za Simba kusaka bao la pili hazikufanikiwa licha ya wenyeji Fountain Gate kubaki 10 uwanjani katika dakika za lala salama baada ya kipa wao, Noble John kupewa kadi ya pili ya njano na kulazimika kutoka nje.
Katika kuhakikisha lango lao linapata ulinzi, Fountain Gate waliamua kumfanya mchezaji wa ndani Hashim Omar kuwa kipa katika dakika zilizobaki lakini Simba hawakuweza kupata bao la pili licha ya kulisaka kwa nguvu nyingi.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, Dodoma Jiji ililala kwa bao 1-0 mbele ya Pamba FC wakati Prisons iliichapa Mashujaa mabao 2-1 na Azam FC ikailaza KMC mabao 2-0.
Soka Simba yakwama kuishusha Yanga kileleni
Simba yakwama kuishusha Yanga kileleni
Read also
