London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amedai kukatishwa tamaa baada ya timu hiyo kutofanya usajili wowote katika dirisha dogo ingawa amepongeza nidhamu ya timu.
Awali zilikuwapo habari kwamba Arsenal ingesajili mshambuliaji baada ya Gabriel Jesus kupata matatizo ya misuli mwishoni mwa mwezi uliopita wakati Bukayo Saka naye akiwa na tatizo linalofanana na hilo na wote wakishindwa kuiwakilisha timu hiyo.
Arteta alisema dhamira yao ilikuwa wazi kwamba baada ya dirisha la usajili kufunguliwa walitakiwa kuangalia fursa za kusajili ili kuimarisha kikosi kwa kusajili wachezaji ambao wangekuwa msaada kwa timu.
Arteta ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja kabla ya Arsenal kujitupa dimbani kuikabili Newcastle katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la EFL itakayopigwa kesho Jumatano.
“Kutokana na wachezaji kuwa majeruhi tulijipa matumaini, hatujayafikia, imetukatisha tamaa lakini hapo hapo tunafahamu kwamba tulitakiwa kusajili aina fulani ya wachezaji na tunatakiwa pia kuwa na nidhamu katika hilo, nafikiri la la nidhamu tuko sawa,” alisema Arteta.
Arteta alisema kuna mchezaji ambaye waliamini angewafanya wawe bora zaidi ingawa alifafanua kuwa katika masuala ya kifedha pia kuna mambo mengi ambayo ni lazima wayasimamie na ndiyo yaliyowafikisha walipofika na kuanzia hapo wanajaribu kuwa bora zaidi.
Arsenal ambayo mwishoni mwa wiki iliyopita iliibugiza Man City mabao 5-1, kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England (EPL) ikiwa imezidiwa na vinara wa ligi hiyo, Liverpool kwa tofauti ya pointi sita.