London, England
Bosi wa waamuzi England, Howard Webb amesema mwamuzi Anthony Taylor alikuwa sahihi kutoa penalti katika mechi ya Arsenal na Brighton iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Tukio lililozaa penalti hiyo lilitokana na beki wa Arsenal, William Saliba kucheza nduvyo sivyo wakati wakiwania mpira na Joao Pedro katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi iliyopita.
Baada ya mechi hiyo kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alieleza kusikitishwa na uamuzi huo akidai hakuwahi kuona tukio la aina hiyo katika maisha yake wakati kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler alisema kwamba kwake anadhani ilikuwa penalti ya wazi.
Kwa upande wake Webb, mwamuzi maarufu wa zamani aliyejijengea heshima England na duniani, alisema anaunga mkono uamuzi wa Taylor kutoa penalti.
Webb alifafanua kwamba tukio lililotokea si tu lilikuwa kosa bali halikuwa la kawaida kwa wachezaji wote wawili kuwania mpira wa juu na beki wa Arsenal kuchelewa kuupiga kichwa na kusababisha adhabu iliyotolewa.
“Unachokiona katika mazingira yaliyojitokeza ni wachezaji wawili kwenda juu kuuwahi mpira, Pedro anaupiga mpira kichwa na Saliba haupigi mpira kichwa anakwenda kwenye kichwa cha Pedro akiwa amechelewa,” alisema Webb.
Webb alisema kwamba inapotokea mchezaji akaonekana wazi anaucheza mpira au anaupiga mbali kwa kichwa hapo utakuwa unazungumzia jambo jingine lakini hicho si kilichotokea.
