Paris, Ufaransa
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa aliyeiwezesha timu hiyo kubeba Kombe la Dunia mwaka 2018, Didier Deschamps amesema ataachana na timu hiyo baada ya fainali za Kombe la
Dunia 2026.
Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitafanyika nchini Marekani, Canada na Mexico na huo ndio utakuwa mwisho wa kocha huyo ambaye amekuwa akiinoa timu hiyo tangu mwaka 2012 alipobeba majukumu hayo kutoka kwa Laurent Blanc.
Deschamps, 56 ndiye kocha aliyeinoa timu ya Ufaransa kwa kipindi kirefu ambapo mbali na Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, pia ameiwezesha kubeba Kombe la Ulaya 2016 nchini Ufaransa na kuifikisha hatua ya fainali kwenye Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
“Mwaka 2026 itakuwa ndio mwisho, hilo katika kichwa changu lipo wazi, nimemaliza kipindi changu nikiwa mwenye hamasa na matamanio yale yale ya kuendelea kuiweka Ufaransa juu,” alisema Deschamps.
Kocha huyo alifafanua kwamba mtu anatakiwa kufika mahali aseme siendelei, na kuna maisha baada ya jambo fulani na kwake la muhimu ni kuiona Ufaransa inakuwa juu kama ambavyo imekuwa kwa miaka mingi.
Deschamps, kiungo na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, mwenye rekodi ya kuichezea timu hiyo mara 103, ameingia katika orodha ya makocha watatu waliowahi kubeba Kombe la Dunia wakiwa wachezaji na baadaye wakiwa makocha.
Wengine katika orodha hiyo ni Mario Zagallo aliyeweka rekodi hiyo akiwa na timu ya taifa ya Brazil na Franz Beckenbauer aliyekuwa na timu ya taifa ya Ujerumani.