Na mwandishi wetu
Yanga imefufua matumaini yake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa TP Mazembe ya DR Congo mabao 3-1 katika mechi ya Kundi A iliyopigwa leo Jumamosi kwenye dimba la Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi nne na kujinasua mkiani ikiishusha Mazembe yenye pointi mbili, timu nyingine za kundi hilo ni vinara Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria.
Mazembe ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 16 lililofungwa kwa penalti na kipa Aliufati Badara, penalti hiyo ilitolewa baada ya Shedrack Boka kumkwatua Ibrahim Keita katika eneo la hatari.
Boka alisawazisha makosa yake dakika ya 33 baada ya kutoa pasi iliyozaa bao la kusawazisha la Yanga lililofungwa Clement Mzize kwa shuti kali lililomshinda kipa Badara.
Dakika nne baada ya bao hilo, Boka aliambaa na mpira upande wa kushoto na kumpasia Stephane Aziz Ki ambaye kwa mshangao akiwa karibu kabisa na kipa wa Mazembe alishindwa kufunga bao
Yanga iliendelea kulisakama lango la Mazembe na dakika ya 56 Aziz Ki alirekebisha makosa yake kwa kuipatia Yanga bao la pili akiitumia vizuri pasi ya Khalid Aucho.
Mazembe kabla hawajatulia walijikuta wakipachikwa bao la tatu lililofungwa na Mzize baada ya Mudathir Yahya kumnyang’anya mpira beki mmoja wa Mazembe na kumpasia Prince Dube aliyempasia Mzize.
Kimataifa Yanga yainyuka Mazembe 3-1
Yanga yainyuka Mazembe 3-1
Read also
