Na mwandishi wetu
Yanga imeendelea kutoa dozi kubwa katika Ligi Kuu NBC baada ya kuitandika Fountain Gate FC mabao 5-0 au mkono katika mechi iliyopigwa Jumapili hii Desemba 29, 2024 kwenye dimba la KMC, Dar es Salaam.
Dozi hiyo ambayo ni ya tatu mfululizo imesababisha timu hiyo kulivunja benchi zima la ufundi kuanzia kocha mkuu Mohamed Muya na wasaidizi wake wote.
Kabla ya ushindi huo, Yanga ilitoa dozi nyingine mbili kubwa kwenye mechi za ligi hiyo dhidi ya Dodoma Jiji na Tanzania Prisons ambazo kila moja ililala kwa mabao 4-0.
Yanga ilianza kuandika bao la kwanza dakika ya 16 mfungaji akiwa Pacome Zouzoua ambaye aliitumia vizuri pasi ya Shadrack Boka ambaye naye aliinasa pasi ya Mudathir Yahya.
Mudathir aliiandikia Yanga bao la pili dakika ya 40 kwa mpira uliotokana na kona ya Aziz Ki na kumkuta Prince Dube aliyeurudisha kwa Clement Mzize ambaye naye alimpasia kabla ya kutua miguuni kwa mfungaji.
Katika dakika ya 45 juhudi za Aziz Ki aliyeuwahi mpira ulioonekana kama hauna mwenyewe na kumpasia Mzize aliyempasia Pacome ambaye aliiandiki Yanga bao la tatu.
Dakika nane baada ya kuanza kipindi cha pili, Yanga iliandika bao la nne lililotokana na shuti la Pacome ambaye alitangazwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Pacome alifumua shuti lililomshinda kipa wa Fountain Gate, John Nobo na kugonga mwamba wa juu kabla ya kurudi uwanjani na beki Jackson Shija kujifunga wakati akiokoa.
Zikiwa zimebakia dakika tatu kabla ya mpira kumalizika, Clement Mzize alihitimisha karamu ya mabao ya Yanga kwa kuandika bao la tano akiitumia pasi ya Salum Aboubakar ‘Sure Boy’.
Kwa ushindi huo Yanga imezidi kuwasogelea vinara wa ligi hiyo Simba baada ya kufikisha pointi 39 ikiwa nafasi ya pili katika mechi 15 sawa na Simba yenye pointi 40.
Wakati Yanga wakifurahia kuisogelea Simba hali ni mbaya kwa Fountain Gate ambao baada ya kipigo hicho walitoa taarifa ya kulivunja benchi zima la ufundi kuanzia kocha mkuu.
Soka Yanga yaipiga mkono Fountain Gate
Yanga yaipiga mkono Fountain Gate
Read also
