Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema kwamba klabu hiyo ipo katika hatari ya kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Man City ina rekodi ya kuvutia kwenye michuano hiyo mikubwa ya klabu barani Ulaya yenye hadhi na utajiri ikiwa hadi sasa inafuzu na kushiriki mara ya 14 mfululizo.
Hofu iliyopo sasa ni nafasi ya timu hiyo kwa msimu ujao wa 2025-26 kwa kuwa inashika nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu England (EPL) baada ya kucheza mechi 17.
Katika taratibu za Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) England ina hadhi ya juu ikiwa na nafasi tano za kushiriki michuano hiyo msimu ujao na kwa msimamo wa EPL ulivyo sasa, Man City haina nafasi.
“Nilipolisema hili hapo kabla watu walicheka, walisema kwamba kufuzu ligi ya mabingwa si mafanikio makubwa lakini mimi nafahamu hilo kwa sababu imekuwa ikitokea kwa klabu za hii nchi, walitawala soka kwa miaka mingi lakini baadaye walishindwa kufuzu ligi ya mabingwa,” alisema Pep.
Pep aliongeza kwa kusema kwamba timu moja ambayo imekuwa kwenye ligi ya mabingwa kwa miaka mingi ya nyuma ni Man City lakini lilizo wazi kwa sasa ni kwamba wapo kwenye hali ya hatari.
Man City leo Alhamisi ya Desemba 26, 2024 itakuwa mwenyeji wa Everton na kufuatiwa na mechi ya ugenini dhidi ya Leicester itakayochezwa Desemba 29 na Januari 4 watauanza mwaka mpya wa 2025 kwa mechi dhidi ya West Ham.
Timu zote hizo tatu zinazocheza na Man City nazo haziko vizuri hivyo huenda ukawa mwanzo mzuri wa mabingwa hao watetezi wa EPL kuonesha ubora wao uliozoeleka kwa misimu kadhaa iliyopita.