Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesisitiza kwamba alikuwa sahihi kumuweka kando mshambuliaji Marcus Rashford kwenye kikosi na Man United na hajutii uamuzi huo.
Man United imetolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Carabao baada ya kuchapwa mabao 4-3 na Tottenham Hotspur na Amorim amesema kwamba hajutii lolote kuhusu Rashford.
Mechi dhidi ya Spurs ni ya pili kwa Rashford kukosekana kwenye kikosi cha timu hiyo, awali aliachwa kwenye mechi dhidi ya Man City ambayo Man United ilishinda kwa 2-1.
Jumanne iliyopita, Rashford alinukuliwa akisema kwamba yupo tayari kuondoka Man United kwa ajili ya changamoto mpya kwingineko kauli iliyomaanisha kwamba mchezaji huyo anaweza kuondoka wakati wowote.
Baada ya Man United kufungwa na Spurs, Amorim aliulizwa iwapo anajutia kumuacha Rashford katika mechi hiyo na kama atabadili uamuzi huo, naye akajibu hajutii na anasimamia msimamo wake huo.
“Najiona niliyefanya jambo sahihi kwa timu, haijawahi kuwa kosa, ni lazima tufanye maamuzi, nafikiri haikuwa kosa kwa sababu wakati wote nafanya kilicho bora kwa ajili ya timu kwa jinsi ninavyoyaona mambo,” alisema Amorim.
Ikicheza dhidi ya Tottenham bila ya Rashford, Man United baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-0 ilipambana na hatimaye kupata mabao mawili kabla ya Spurs kuongeza la nne na United kupata bao jingine moja.
