Doha, Qatar
Winga wa Real Madrid, Vinícius Jr ametwaaa tuzo ya Fifa ya mwanasoka bora wa mwaka kwa wanaume wakati tuzo hyo kwa wanawake imekwenda kwa kiungo wa Barcelona, Aitana Bonmatí.
Kwa Vinicius tuzo hiyo inakuwa faraja kubwa baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Ballon d’Or Oktoba mwaka huu, tuzo ambayo ilibebwa na Rodri wa Man City.
Vinicius, 24, alionesha wazi kukerwa kwa kutoshinda Ballon d’Or lakini hatimaye Jumanne hii imekuwa siku nzuri kwake alipobeba tuzo ya Fifa katika hafla zilizofanyika mjini Doha.
Katika msimu uliopita, Vinicius ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Brazil, alitoa mchango mkubwa kwa Real Madrid hadi kutwaa mataji ya La Liga na Ligi ya Mabingwa, akifunga mabao 24 na kutoa asisti 11.
Vinicius hadi kutwaa tuzo hiyo alipata kura 48 akimbwaga Rodri ambaye alipata kura 43 wakati staa mwingine wa Real Madrid Jude Bellingham yeye aliyepata kura 37.
Kwa upande wa tuzo ya bao la mwaka maarufu Puskas Award, tuzo hiyo ilichukuliwa na mshambuliaji wa Man United, Alejandro Garnacho kwa bao alilofunga kwa staili ya tikitaka kwenye mechi dhidi ya Everton iliyopigwa Novemba na Man United kutoka na ushindi wa mabao 3-0.
Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti ameshinda kipengele cha kocha bora wa mwaka akibebwa na mafanikio ya timu yake iliyobeba mataji ya Ligi Kuu Hispania au La Liga pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tuzo hiyo kwa upande wa wanawake imechukuliwa na kocha wa zamani wa Chelsea, Emma Hayes ambaye kwa sasa anainoa timu ya soka ya wanawake ya Marekani.
Hayes ambaye pia ni mshindi wa Ballon d’Or, ameiwezesha Chelsea kubeba taji la Super League kabla ya kubeba medali ya dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris akiwa na timu ya Marekani.
Kimataifa Vinícius atwaa tuzo ya Fifa
Vinícius atwaa tuzo ya Fifa
Read also
