Na mwandishi wetu
Haiishi mpaka iishe, ndicho kilichotokea baada ya Kibu Denis kufunga mabao mawili na kuiwezesha Simba kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya CS SFaxien ya Tunisia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo Jumapili, Desemba 15, Simba ililazimika kusubiri hadi dakika za jioni kupata bao la pili na kutoka uwanjani na pointi tatu.
Ushindi huo uliopatikana kwa mbinde unakuwa wa pili kwa Simba katika mechi zake tatu za michuano hiyo, ilianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bravos du Maquis ya Angola kabla ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya SC Constantine ya Algeria.
Simba leo iliianza vibaya mechi yake baada ya SFaxien kuziona nyavu za timu hiyo mapema katika dakika ya tatu ya mchezo huo kwa bao lililofungwa na Hazem Hajhasen.
Mfungaji aliyatumia makosa ya beki Che Malone Fondoh ambaye akiwa katika umiliki wa mpira alimrudishia pasi dhaifu kipa wake Musa Camara na mpira huo kuwahiwa na mfungaji aliyeujaza wavuni.
Kuingia kwa bao hilo hakukuiyumbisha Simba ambayo dakika takriban tatu baadaye ilipata bao la kusawazisha lililofungwa na Kibu kwa kichwa akiunganisha mpira uliopigwa na Jean Ahoua.
Mpira uliozaa bao hilo ulitokana na juhudi za Kibu ambaye alichezewa rafu na ndipo Ahoua alipopiga mpira huo kiufundi kwa kumchungulia Kibu ambaye aliruka juu na kuujaza wavuni.
Dakika ya 26 Simba walifanya shambulizi lililotokana na mpira wa krosi uliopigwa na Ahoua na Lionel Ateba akaunganisha kwa kichwa lakini mpira huo ukatoka nje.
Simba tena dakika ya 33 ilifanya shambulizi jingine kuanzia kwa Shomari Kapombe akiwa upande wa kulia alipiga krosi na Ahoua kuunganisha kwa kupiga shuti lililotoka nje.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini hadi mapumziko matokeo yalibaki kuwa ya sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kocha wa Simba, Fadlu Davids alianza kufanya mabadiliko akimtoa Ateba na nafasi yake kuingia Steven Mukwala kabla ya kumtoa Ahoua na kumuingiza Joshua Mutale na Che Malone ambaye nafasi yake aliingia Karaboua.
Mabadiliko hayo yaliiongezea uhai Simba kwa kuendelea kumiliki mpira na kufanya mashambulizi huku SFaxien wakiwa na kazi ya kujihami na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Kocha wa Simba aliendelea na mabadiliko kwa kuwatoa Debora Fernandez na nafasi yake kuingia Kagoma kabla ya kumtoa nahodha Mohamed Hussein na kumuingia Valentino Nouma.
Kasi ya mashambulizi iliendelea kwa Simba huku SFaxien wakiwa na kazi ya kujihami zaidi na kuchelewesha muda na ndipo mwamuzi alipoongeza dakika saba kufidia muda uliokuwa ukipotea.
SFaxien hata hivyo waliendelea kuchelewesha muda kwa kujiangusha na zaidi ilikuwa kwa kipa wao Aymen aliyekuwa akilala chini mara kwa mara.
Simba waliendelea kupambana kabla ya kupata bao katika dakika hizo za nyongeza (dakika ya nane) baada ya Kibu kuunganisha kwa kichwa krosi ya Donald Ngoma.
Kuingia kwa bao hilo kuliamsha shangwe kwa mashabiki wa Simba na kuzua tafrani kwa mashabiki wa SFaxien waliokuwa wakipambana na wale wa Simba kwa kurushiana viti.
Wakati huo huo baadhi ya wachezaji na benchi zima la SFaxien nao walianza kumkabili mwamuzi kwa kuamini kwamba aliibeba Simba kwa namna alivyoongeza muda.
Kimataifa Kibu aibeba Simba Kwa Mkapa
Kibu aibeba Simba Kwa Mkapa
Read also
