Na mwandishi wetu
Prince Dube ameacha kilio mjini Lubumbashi baada ya kufunga bao na kuiwezesha Yanga kutoka sare ya 1-1 na TP Mazembe ya mjini Lubumbashi, DR Congo katika mechi ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi hiyo iliyopigwa leo Jumamosi Desemba 14, 2024 mjini Lubumbashi, matokeo yake yanaibua matumaini kwa Yanga ambayo katika mechi zake tatu za kundi hilo imepoteza mbili dhidi ya Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria.
Sare hiyo hata hivyo bado haijaweza kuitoa Yanga mkiani mwa kundi hilo kwani hadi sasa ina pointi moja tu wakati Mazembe inayoshika nafasi ya tatu ina pointi mbili.
Mazembe waliandika bao lao dakika tano kabla ya timu kwenda mapumziko lililofungwa na Check Fofana aliyeingia akitokea benchi akiunganisha kwa kichwa krosi ya Johnson.
Awali mpira huo uliokolewa lakini ulikuwa ushavuka mstari wa goli na hivyo mwamuzi kuamuru uwekwe kati.
Yanga ilianza kulisaka bao hilo kwa udi na uvumba kuanzia kipindi cha pili huku kocha akifanya mabadiliko kadhaa akianza kwa kumtoa kipa Djigui Diarra aliyeumia na nafasi yake kuingia Aboubakar Khomeiny.
Mabadiliko hayo yaliendelea kwa kumtoa Maxi Nzengeli na kumuingiza Clement Mzize pamoja na Mudathir Yahya ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Stephane Aziz Ki.
Baadaye akatoka Kennedy Musonda na nafasi yake kuingia Dube kabla ya Duke Abuya naye kutolewa na nafasi yake kuingia Clatous Chama.
Mabadiliko hayo hayakuwazuia Mazembe kuichachafya Yanga ingawa Yanga nao walionekana kupata uhai katika safu ya ushambuliaji na hatimaye kupata bao hilo pekee katika dakika ya nne ya nyongeza baada ya dakika 90 za kawaida kukamilika.
Dube alifunga bao hilo baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Mazembe na hatimaye mshambuliaji huyo kufumua shuti lililompita kipa Alioufati Badara.
Dube ambaye amekuwa akiandamwa na ukame wa mabao alilifurahia bao hilo kwa kupiga magoti huku hali ikiwa ya huzuni kwa Mazembe waliokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Kuanzia mashabiki waliojazana uwanjani, wachezaji wa ndani, wa akiba na benchi zima la timu hiyo wengi wao walilala chini wakilia na kuhuzunika wasiamini kilichowakuta.
Kimataifa Dube aacha kilio Lubumbashi
Dube aacha kilio Lubumbashi
Read also
