Na mwandishi wetu
Yanga imejikuta pagumu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 2-0 na MC Alger ya Algeria katika mechi ya Kundi A na hicho kuwa kipigo cha pili kwenye michuano hiyo.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii Desemba 7, 2024, Yanga ikiwa ugenini ilishindwa kutumia faida ya wenyeji kucheza bila mashabiki uwanjani na kujikuta ikitoka uwanjani na matokeo hayo mabaya.
Kipigo hicho ni cha pili kwa Yanga kwani kabla ya hapo ililala kwa mabao kama hayo mbele ya Al Hilal Omdurman ya Sudan katika mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo.
Yanga iliuanza mchezo kwa kuonesha uhai ikifanya mashambulizi na kuwadhibiti MC katika kipindi cha kwanza na kutoka uwanjani bila kufungana lakini mambo yalianza kuwa mabaya kipindi cha pili.
MC waliandika bao la kwanza katika dakika ya 65 ya mchezo huo mfungaji akiwa nahodha wa timu hiyo Ayoub Abdellaoui akiutumia vizuri mpira wa adhabu uliopigwa na Mohamed Halaimi.
Abdellaoui aliwazidi ujanja mabeki wa Yanga kabla ya kumtungua kipa Djigui Diarra na kuipa timu yake bao la kwanza.
Mambo yaliwaharibikia Yanga katika dakika za lala salama baada ya Soufian Bayazid kuandika bao la pili akiitumia pasi ya Kamel Hamid.
Kwa matokeo hayo Yanga inashika mkia katika kundi lake ikiwa haina pointi hata moja wakati MC wanashika usukani wakiwa na pointi nne na Al Hilal wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu huku TP Mazembe wakiwa nafasi ya tatu na pointi yao moja.
Matokeo ya mechi ya Jumapili Desemba 8, 2024 kati ya Al Hilal na TP Mazembe yanaweza kuubadili msimamo wa kundi hilo na haitoshangaza MC ikienguliwa kileleni.
Kimataifa MC Alger yaipiga Yanga 2-0
MC Alger yaipiga Yanga 2-0
Read also