Madrid, Hispania
Baada ya Kylian Mbappe kukosa penalti kwa mara ya pili, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amedai bado ana imani mshambuliaji huyo ana uwezo wa kufanya vizuri na ataendelea kuwa mpigaji penalti.
Mbappe alikosa penalti jana Jumatano katika mechi ya La Liga dhidi ya Athletic Bilbao na hivyo kushindwa kuiokoa timu yake ambayo mwishowe ililala kwa mabao 2-1.
Athletic ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 53 lililofungwa na Alex Berenguer na Mbappe akapata nafasi ya kusawazisha kupitia penalti lakini shuti alilopiga liliokolewa na kipa Julen Agirrezabala.
Mbappe hata hivyo juhudi zake zilizaa bao la kusawazisha lililofungwa na Jude Bellingham kufuatia shuti la Mbappe lililookolewa kabla ya kumkuta mfungaji.
Athletic hata hivyo walineemeka na makosa ya Federico Valverde katika dakika za lala salama baada ya kupata bao lililofungwa na Gorka Guruzeta.
Hii ni mara ya pili katika kipindi kisichozidi wiki moja kwa Mbappe kukosa penalti, awali alikosa penalti wiki iliyopita katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool, mechi ambayo Real Madrid ililala kwa mabao 2-0.
“Sijazungumza na Mbappe na siwezi katu kumfanyia tathmini mchezaji kupitia penalti, kuna wakati unafunga na kuna wakati unakosa, najua amehuzunika na kukatishwa tamaa lakini lazima tuangalie mbele,” alisema Ancelotti.
Ancelotti pia alisema kwamba hata Valverde ana huzuni na amekatishwa tamaa kama ilivyo kwa Mbappe lakin naye ni mchezaji mkubwa na watu hufanya makosa kwenye soka.
Mbappé hadi sasa ana mabao 10 katika mechi 20 za Real Madrid tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu lakini amejikuta akishutumiwa mara kadhaa kwa kinachodaiwa kuwa hayuko katika kiwango bora.
Akizungumzia kukosa kwake penalti, Mbappe alisema kwamba anawajibika kwa kila kitu lakini akasisitiza kwamba ni wakati wa kubadilika na kuonesha yeye ni nani.
Ancelotti kwa upande mwingine alisema kwamba Mbappe ataendelea na majukumu ya upigaji wa penalti katika timu hiyo pamoja na VinÃcius Júnior na Bellingham.
