Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amemsifia mshambuliaji wake Kylian Mbappe akimtaja kuwa ni hatari baada ya kufunga bao katika ushindi wa 2-0 walioupata jana Jumapili dhidi ya Getafe.
Mbappe amekuwa akipitia kipindi kigumu cha lawama tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu baada ya kuandamwa na ukame wa mabao huku baadhi ya wachambuzi wakidai hayuko katika ubora uliozoeleka.
Baada ya kufunga bao hiyo jana Ancelotti alisema kwamba hicho ndicho wanachokihitaji kutoka kwa mshambuliaji huyo.
Katika mechi hiyo, Jude Bellingham ndiye aliyeifungia Real Madrid bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 30 kabla ya kutoa pasi iliyozaa bao la pili lililofungwa na Mbappe dakika nane baadaye.
Ushindi huo umeifanya Real Madrid kujiimarisha katika nafasi ya pili kwenye La Liga wakiwa wamezidiwa na vinara Barca kwa tofauti ya pointi moja ingawa Real Madrid wana mechi moja pungufu.
“Mbappe alikuwa hatari kama anavyokuwa siku zote, alifunga bao muhimu lililosaidia kutufanya tuutawale mchezo vizuri na akapata nafasi katika kipindi cha pili, alikuwa shapu na hicho ndicho tunachohitaji kutoka kwake,” alisema Ancelotti.
Mbappe amefunga mabao mawili tu katika mechi tisa na alikosa penalti katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool katikati ya wiki lakini sasa ni kama ameanza kurudi katika makali yaliyozoeleka.
