Manchester, England
Klabu ya Manchester United hatimaye imemteua Ruben Amorim (pichani) kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo akichukua nafasi iliyoachwa na Erik ten Hag aliyetimuliwa.
Amorim mwenye umri wa miaka 39 ambaye anatokea Sporting Lisbon ya Ureno, amesaini mkataba unaofikia ukomo Juni 2027 na anatarajia kutua rasmi Old Trafford yalipo makazi ya Man United Novemba 11.
Kwa mantiki hiyo kocha wa muda, Ruud van Nistelrooy aliyekabidhiwa majukumu mara baada ya kutimuliwa kwa Ten Hag Jumatatu iliyopita, ataendelea kufanya kazi hiyo kwa mechi tatu zijazo.
Tetesi kuhusu Amorim zilianza kusikika katika siku za karibuni ambapo kocha mwingine ambaye jina lake pia lilikuwa likitajwa mara kadhaa ni Xavi Hernandez aliyekuwa akiinoa Barcelona.
Amorim anakuwa kocha wa sita wa kudumu wa Man United tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson, kocha ambaye aliinoa klabu hiyo kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka 26 kabla ya kung’atuka mwaka 2013.
Sporting walithibitisha Amorim kwenda Man United na kubainisha kwamba klabu hiyo ilikubali kuuvunja mkataba wa sasa wa Amorim na kutoa kiasi cha fedha kama sehemu ya makubaliano hayo.
Amorim anatajwa kuwa mmoja wa makocha wenye umri mdogo ambaye ameanza kuheshimika katika soka Ulaya, mtihani wake wa kwanza katika Ligi Kuu England akiwa kwenye benchi la Man United utakuwa Novemba 24 dhidi ya Ipswich Town.
Kimataifa Amorim kocha mkuu Man United
Amorim kocha mkuu Man United
Read also
