Na mwandishi wetu
Yanga imefanikiwa kuushika usukani wa Ligi Kuu NBC msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa Singida BS bao 1-0 katika mechi iliyochezwa leo Jumatano kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Kwa ushindi huo Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo wamefikisha pointi 24 na kuwazidi Singida BS kwa pointi mbili ingawa Singida imecheza mechi tisa wakati Yanga hadi sasa imecheza mechi nane.
Bao hilo pekee la Pacome lilipatikana katika dakika ya 67 baada ya mchezaji huyo kufumua shuti kali la mguu wa kushoto lililompita kipa wa Singida BS, Metacha Mnata.
Metacha ambaye aliwahi kuichezea Yanga, licha ya kufungwa bao hilo lakini mara kadhaa alikuwa mwiba kwa safu ya ushambulizi ya Yanga na haikushangaza Yanga kupata bao hilo pekee licha ya mashambulizi kadhaa waliyoyafanya.
Yanga ilipata pigo la mapema baada ya beki wake wa kushoto mwenye uwezo mkubwa wa kupanda kupeleka mashambulizi, Shedrack Boka kuumia dakika ya saba na baadaye kutolewa dakika ya 17 na nafasi yake kuingia Nickson Kibabage.
Kibabage hakuwangusha Yanga, dakika ya 31, aliambaa vyema na mpira akitokea upande wa kushoto wa timu yake na kumpa pasi ya chinichini Aziz Ki ambaye shuti lake liligonga mwamba kabla ya kuokolewa na Metacha.
Singida BS walijibu shambulizi hilo dakika 10 baadaye kwa kufanya shambulizi lililotokana na mpira wa kurushwa ambao D Camara aliuunganisha kwa kichwa na Elvis Rupia naye akapiga tena kwa kichwa na mpira kutoka sentimita chache juu ya lango la Yanga.
Yanga walifanya shambulizi tena dakika ya 61, Clatous Chama alimpasia mpira Aziz Ki ambaye alipiga shuti la juu na Metacha kuonesha umahiri wake kwa kuufuata mpira huo juu na kuutoa kona ambayo haikuzaa matunda.
Mambo yaliendelea kuwaharibikia Yanga ambao walilazimika kumtoa Kibabage na nafasi yake kuingia Ibrahim Bacca baada ya Kibabage kuumia.
Soka Yanga yashika usukani ligi kuu
Yanga yashika usukani ligi kuu
Read also