Paris, Ufaransa
Kiungo wa Man City na timu ya taifa ya Hispania, Rodri ameibuka kinara wa tuzo ya Ballon d’Or 2024 akimbwaga mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Vinicius Junior.
Rodri na Vinicius ni miongoni mwa majina yaliyochomoza na kutajwa zaidi na wachambuzi wa soka kwamba mmoja wao angeibuka kinara wa tuzo hiyo iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumanne.
Sambamba na wawili hao jina jingine ambalo lilionekana kutajwa mara kadhaa ni la mshambuliaji mwingine wa Real Madrid na timu ya taifa ya England, Jude Bellingham.
Baada ya Rodri kutangazwa mshindi waliofuata baada yake ni Vinicius na Bellingham huku Rodri akibebwa na mafanikio yake Man City waliobeba taji la Ligi Kuu England na Hispania alikobeba taji la Ulaya maarufu Euro 2024.
Inadaiwa Real Madrid haikuwakilishwa katika tuzo hizo baada ya kubaini kwamba Vinicius aliyepewa nafasi kubwa hakuwa kinara wa tuzo hiyo.
Awali akizungumzia kitendo cha Real Madrid kutowakilishwa kwenye tuzo hiyo, kocha wa Man City, Pep Guardiola ambaye kama ilivyo Rodri naye anatokea Hispania alisema yote ni sawa.
“Kama Real Madrid watataka kwenda sawa, kama hawatataka pia sawa, kama watataka kutoa pongezi sawa kama hawatataka kutoa pongezi pia hilo ni sawa,” alisema Pep.
Pep alifafanua kwamba unapokuwa wa pili au wa tatu katika tuzo hizo maana yake ni kwamba umefanya kitu cha kipekee, maana yake ni kwamba umekuwa na mwaka mzuri na unatakiwa uridhike.
Rodri ni mchezaji wa kwanza wa Man City kushinda tuzo ya Ballon d’Or na ni mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu England kushinda tuzo hiyo tangu Cristiano Ronaldo ashinde tuzo hiyo mwaka 2008.
Kimataifa Rodri ambwaga Vinicius Ballon d’Or
Rodri ambwaga Vinicius Ballon d’Or
Read also
