Riyadh, Saudi Arabia
Mshambuliaji nyota wa Brazil aliyekuwa majeruhi kwa takriban mwaka mmoja, Neymar hatimaye amerejea uwanjani kwa mara ya kwanza na kuiwakilisha timu yake ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
Neymar alicheza mechi hiyo Jumatatu hii dhidi ya Al Ain, aliingia akitokea benchi katika dakika ya 77 na kuchukua nafasi ya Nasser Al Dawsari wakati huo Al Hilal ikiwa inaongoza kwa mabao 5-3.
Mara baada ya kuingia Neymar nusura aisaidie timu yake kupata bao la sita baada ya kucheza pasi kadhaa na Aleksandar Mitrovic kabla ya kufumua shuti lililotoka kidogo nje ya lango.
Baada ya mechi hiyo iliyoisha kwa Al Hilal kutoka na ushindi wa mabao 5-4, Neymar alisema anajisikia furaha na wakati wote amekuwa na timu nzuri lakini zaidi ana furaha ya kurudi tena uwanjani.
Neymar nyota wa zamani wa PSG ya Ufaransa aliumia goti wakati akiiwakilisha Brazil dhidi ya Uruguay na kufanyiwa upasuaji Novemba mwaka jana na tangu hapo amekuwa nje ya uwanja kabla ya kurejea Jumatatu.
Aljiunga na Al Hilal Agosti mwaka jana akitokea PSG kwa ada ya Euro 90 milioni lakini aliichezea timu yake hiyo mpya mechi tano tu kabla ya kuumia na sasa amerejea na kupongezwa na timu yake ya zamani ya Santos ya kwao Brazil.
“Ni zaidi ya miezi 12 ya kuwa nje ya uwanja, akiwa na shauku kubwa ya kurudi ili kufanya kile anachokipenda zaidi,” ilieleza taarifa ya Santos kupitia mitandao ya kijamii.
Wakati wote akiwa majeruhi, Neymar mbali na kushindwa kuiwakilisha Al Hilal pia alishindwa kuiwakilisha Brazil kwenye fainali za Copa America zilizofanyika Marekani na Argentina kubeba kombe.
Kwa sasa inasubiriwa kuona kama mchezaji huyo ataweza kuiwakilisha Brazil kwenye mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Venezuela na Uruguay zitakazopigwa Novemba mwaka huu.
Kimataifa Neymar arejea uwanjani
Neymar arejea uwanjani
Read also
