Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Yanga umetangaza kuwa ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote au taasisi kutengeneza, kuagiza au kusambaza bidhaa zozote zenye nembo ya Yanga bila ruhusa.
Taarifa ya klabu hiyo kutoka idara ya sheria iliyopatikana Alhamisi hii, pia imefafanua kuwa ni kinyume cha sheria kwa wafanyabiashara wa jumla na rejareja kuuza bidhaa zozote zenye nembo ya klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bidhaa hizo ili ziweze kuuzwa na wafanyabiashara hao ni lazima ziwe zimesambazwa na mshirika rasmi wa klabu hiyo ambaye ni kampuni ya GSM.
Agizo la klabu hiyo limekuja ikiwa takriban mwaka mmoja umepita tangu polisi jijini Dar es Salaam wakamate kontena mbili zenye jezi zinazodaiwa kuwa na nembo ya Yanga, Simba, Azam FC na Taifa Stars.
Sambamba na katazo la kuuza na kusambaza bidhaa zenye nembo ya klabu hiyo, taarifa ya Yanga pia imepiga marufuku kwa taasisi yoyote kutumia nembo ya Yanga kwenye matangazo yake ya aina yoyote bila ridhaa ya klabu hiyo.
Yanga wameeleza kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa hakimiliki za klabu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayehusika.
Katika kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi na wananchi wote, klabu hiyo imeahidi kutoa zawadi nono kwa yeyote atakayetoa taarifa za kuwabaini wanaojihusisha na shughuli hizo ambazo klabu hiyo umezitaja kuwa ni haramu.
Hakimiliki Marufuku kuuza jezi zenye nembo ya Yanga
Marufuku kuuza jezi zenye nembo ya Yanga
Read also