Barcelona, Hispania
Rais wa klabu ya Barcelona, Joan Laporta amesema klabu yake imekataa dau la Dola 270 milioni kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wao, Lamine Yamal katika majira ya kiangazi.
Laporta ingawa hakuweka wazi klabu iliyowasilisha ofa hiyo lakini inaaminika kuwa PSG ya Ufaransa ndiyo iliyokuwa ikimtaka mshambuliaji huyo ili kuziba pengo la Kylian Mbappe ambaye alihamia Real Madrid.
Kauli ya kigogo huyo wa Barca imekuja wakati huu klabu yake ikiweka wazi kuhusu uamuzi wa kukubali kuwaachia baadhi ya wachezaji waondoke na kukana kukabiliwa na tatizo lolote la kifedha.
“Kuna ambao wanadhani kwamba tumewaacha wachezaji waondoke ili kuweka sawa masuala ya kifedha, hilo haliko hivyo, wachezaji ambao wameondoka sababu za kufanya hivyo ni za kiuchezaji,” alisema Laporta.
Laporta aliwatolea mfano wachezaji Ousmane Dembele na Marc Giui akidai kwamba hawatokuwa na mambo mazuri katika klabu nyingine kama ilivyokuwa wakati wakiwa wanaichezea Barca.
Alifafanua kuwa wanajua wanachokifanya katika soko la usajili na wachezaji wanaowataka ni wale ambao wapo katika ubora na ambao wanataka kubaki na klabu hiyo na wamedhihirisha jambo hilo.
Tangu kuibuka kwake mwaka 2023 akiwa na miaka 15, Yamal amekuwa na namba ya uhakika katika kikosi cha Barca pamoja na timu ya taifa ya Hispania.
Tayari ana rekodi ya kucheza zaidi ya mechi 60 za Barca na alitoa mchango mkubwa kwa timu ya taifa ya Hispania hadi kubeba taji la Uefa Euro 2024 nchini Ujerumani baada ya kuibwaga England.
