Manchester, England
Man United imemkatia rufaa nahodha wake Bruno Fernandes baada ya kupewa kadi nyekundu katika mechi ya Jumapili dhidi ya Tottenham Hotspur na sasa mchezaji huyo ameepuka adhabu.
Fernandes alipewa kadi nyekundu ya moja kwa moja mara tu baada ya kumchezea rafu kiungo wa Spurs, James Maddison na ilitarajiwa angefungiwa mechi tatu kwa kosa hilo.
Uamuzi wa Man United kumkatia rufaa Fernandes maana yake ni kwamba mchezaji huyo kwa sasa anawekwa kando na adhabu hiyo na Man United itaendelea kumtumia hadi itakapoamuliwa vingine.
Man United wanadai kwamba uamuzi wa kumpa kadi nyekundu Fernandes haukuwa sahihi na sasa mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo atakuwa huru kucheza mechi dhidi ya Aston Villa, Brentford na West Ham.
Wakati Fernandes akitoka uwanjani katika mechi hiyo kwenye dakika ya 42, Man United tayari ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 na hadi mechi inamalizika timu hiyo ililala kwa mabao 3-0.
Hiyo ni mechi ya tatu kwa Man United kupoteza tangu kuanza kwa msimu huu wa 2024-25 wa Ligi Kuu England (EPL).
“Si kweli, ile haikuwa kadi nyekundu, huo ndio mtazamo wangu, nakubali ni faulo, mwamuzi alijaribu kuniambia kwamba nilimgusa na sehemu ya chini ya kiatu, si kweli sikufanya hivyo ni sehemu ya enka ndiyo iliyomgusa,” alisema Fernandes.
Fernandes alisema kwamba kama mwamuzi angeamua kumpa kadi ya njano hapo angekubali lakini zaidi ya hilo si sahihi.
