Na mwandishi wetu
Timu ya Yanga imefanikiwa kutoka uwanjani na pointi tatu mbele ya Ken Gold FC baada ya kuichapa bao 1-0 kaika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Jumatano kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Bao pekee lililoitoa Yanga kimasomaso katika mechi hiyo lilifungwa dakika ya 17 na beki wa kati Ibrahim Bacca ambaye aliunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Stephane Aziz Ki.
Ken Gold ambayo haijashinda hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi msimu huu, ilionekana kuwa kisiki dhidi ya Yanga kwa kuwafanya washambuliaji nyota wa timu hiyo kushindwa kupata mabao.
Matarajio ya Yanga kuongeza mabao baada ya bao la Bacca yalifutwa na ukuta mgumu wa Ken Gold ukiongozwa na mlinda mlango Castro Mhagama ambaye alikuwa kikwazo mbele ya Yanga.
Dakika ya 41, Clement Mzize aliinasa pasi ya Maxi Nzengeli na kuambaa na mpira kabla ya kufumua shuti la chinichini ambalo Mhagama aliliokoa.
Mhagama kwa mara nyingine dakika ya 59 aliokoa shuti la Nzengeli lililotokana na pasi ya Shadrack Boka na kuwa kona iliyopigwa na Clatous Chama na mpira kuokolewa.
Dakika ya 84 tena Mhagama alikuwa kikwazo kwa Yanga akiokoa mpira uliopigwa na Pacome Zouzoua ambao ulikuwa ukielekea golini lakini akaupoza kabla ya kukolewa na beki wake.
Katika dakika ya 86, Ken Gold walifanya shambulizi ambalo nusura lizae bao baada ya Albert Lukindo akiwa karibu na kipa Djigui Diarra kuupiga mpira wa kichwa uliompita Diarra lakini haukuvuka mstari wa goli, tukio lililozua utata kwa Ken Gold kulalamika wakiamini kuwa mpira ulivuka mstari kabla ya kurudi dimba.
Dakika ya 82 mwamuzi alilazimika kumpa kadi ya njano beki wa Ken Gold, Mackenzie Ramadhan baada ya mchezaji huyo kuingia katika mzozo na Boka tatizo likianzia kwa wachezaji hao kugongana wakiwania mpira wa juu.
Baada ya mpira huo Boka alimfuata Mackenzie na kumlaumu kabla ya kumsukuma na Mackenzie akajibu ndipo Kennedy Musonda alipoingilia na kumuondoa Mackenzie.
Ushindi mdogo wa Yanga umeonekana kuwashangaza wengi kwani licha ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha Miguel Gamondi bado timu hiyo ilikwama kuupenya ukuta wa Ken Gold.
Gamondi alianza kwa kuwatoa Mzize na Chama na kuwaingiza Prince Dube na Pacome, baadaye akawatoa Nzengeli na Aziz Ki na kuingia Mudathir Yahya na Musonda na mwisho akamtoa Yao Kouasi na kumuingiza Aziz Andambwile.
Kwa upande wa Ken Gold, kocha Jumanne Chale aliwatoa Mashimo Daud na Albert Lukindo na kuwaingiza Hemed Nassor na Emmanuel Mpuka.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo mambo yamekuwa mabaya kwa Coastal Union ambayo imelala kwa mabao 2-1 mbele ya Namungo.
Soka Yanga yabeba pointi 3 kwa Ken Gold
Yanga yabeba pointi 3 kwa Ken Gold
Read also