Na mwandishi wetu
Yanga imeendeleza ubabe katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibugiza Commercial Bank of Ethiopia (CBE) mabao 6-0 na kufuzu moja kwa moja hadi hatua ya makundi.
Kwa ushindi huo uliopatikana Jumamosi hii Septemba 21 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, Yanga pia imelamba kitita cha Sh milioni 30 ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia ameahidi kutoa Sh milioni tano kwa kila bao linalofungwa kwenye michuano hiyo iwapo timu itatoka na ushindi katika mechi husika.
Baada ya kufanya mashambulizi Yanga ilianza kuzitikisa nyavu za CBE dakika ya 35 kwa bao la Clatous Chama ambaye aliinasa pasi ya Maxi Nzengeli, akamlamba chenga kipa Alemayo na kuujaza mpira wavuni.
Bao hilo halikuubadili mchezo kwa kiasi kikubwa kwani licha ya Yanga kufanya mashambulizi ya hapa na pale lakini CBE walikuwa makini kujihami na hadi mapumziko Yanga walitoka uwanjani na bao hilo pekee.
Moto wa Yanga ulianza kuonekana kipindi cha pili baada Clement Mzize kuambaa na mpira kabla ya kumchambua kipa wa CBE na kuujaza mpira wavuni.
Baada ya hapo Yanga ilifanya mabadiliko, kocha Miguel Gamondi aliwatoa Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Mzize na Chama na kuwaingiza Stephane Aziz Ki, Duke Abuya, Prince Dube na Kennedy Musonda.
Mabadiliko hayo yalizidi kuipa nguvu Yanga ambayo ilipata bao la tatu dakika ya 74 lililofungwa na Aziz Ki akiitumia krosi ya Shedrack Boka ambayo kwanza mpira uliokolewa kabla ya kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.
Baada ya bao hilo Gamondi alimtoa Yao Kouasi na nafasi yake kuingia Dennis Nkane na hapo hapo Yanga ikapata bao la nne lililofungwa na Mudathir Yahya dakika ya 87.
Mudathir ambaye kama kawaida Yanga hushangilia kwa staili ya kupokea simu, alifunga bao hilo baada ya kuinasa pasi ya juu ya Dube, akautuliza mpira kifuani kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni.
Dakika ya 90 Yanga iliandika bao la tano lililofungwa na Abuya kutokana na pasi ya Aziz Ki, dakika ya pili kwenye dakika tatu za nyongeza Yanga iliandika bao la sita lililofungwa na Aziz Ki kwa pasi ya Boka.
Kwa matokeo hayo Yanga inakuwa imefuzu hadi hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0 hiyo ni baada ya ushindi wa awali wa bao 1-0 walioupata wiki iliyopita wakiwa ugenini Ethiopia.
Kimataifa Yanga yaibugiza CBE 6-0
Yanga yaibugiza CBE 6-0
Read also