Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema kuna watu wanaotaka kuona Man City ikitoweka baada ya timu hiyo kukabiliwa na tuhuma za makosa 115 ya uvunjifu wa kanuni za matumizi ya fedha za Ligi Kuu England (EPL).
Man City inaweza kujikuta ikiadhibiwa kwa kunyang’anywa pointi nyingi na hata kushushwa daraja au kufutwa kabisa kwenye EPL kama ikikutwa na hatia ya kuvunja kanuni hizo.
Timu hiyo ambayo katika misimu saba iliyopita ilibeba mataji sita tofauti wakati wote vigogo wake wamekuwa wakikana makosa hayo lakini Pep anaamini wapinzani wao EPL wanachotaka ni kuona timu hiyo ikiadhibiwa.
Ikiwa katika mbio za kulisaka taji la EPL msimu huu wa 2024-25, Jumapili hii Man City watakuwa wenyeji wa Arsenal wakati sakata la tuhuma zinazowakabili likiendelea kusikilizwa huku hatma yake ikisubiriwa kwa shauku kubwa na wadau wa soka duniani kote.
“Samahani ningependa kuitetea klabu yangu hasa katika zama hizi ambazo kila mmoja anatarajia kuona sisi tukishushwa daraja, tukipotea kwenye uso wa dunia, tuna wakari mzuri kuliko wapinzani wetu na ndio maana tunashinda sana,” alisema Pep.
Man City inadaiwa kuvunja kanuni za matumizi ya fedha za EPL kati ya mwaka 2009 hadi 2018 na kwa kipindi hicho timu hiyo imebeba mataji manane ya ligi na mataji mengineyo likiwamo taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mafanikio ya Man City kwa kipindi hicho kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na kampuni ya Abu Dhabi United iliyoinunua klabu hiyo mwaka 2008.
Tuhuma zinazoikabili Man City kwa wakati huo zilifikishwa mbele ya tume huru mwaka 2023 baada ya uchunguzi uliochukua miaka minne.
