Manchester, England
Kiungo wa Man City na timu ya taifa ya Hispania, Rodri (pichani) ameema kwamba wachezaji wapo mbioni kufanya mgomo kutokana na mzigo wa ratiba ngumu yenye mechi nyingi za soka.
Kwa msimu uliopita pekee, Rodri amecheza jumla ya mechi 63 za Man City pamoja na timu yake ya taifa katika msimu ambao ulifikia ukomo Julai 14 baada ya fainali za Kombe la Ulaya au Euro 2024.
Mchezaji huyo msimu huu anakabiliwa na mzigo wa mechi nyingi zaidi kuanzia Man City ambayo itashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ambayo msimu huu itakuwa katika utaratibu mpya.
Zaidi ya hilo pia atashiriki michuano mipya ya klabu ya dunia ambayo itaanza mwezi Juni na hivyo huenda akajikuta akiwa na mzigo wa mechi nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa msimu uliopita.
Alipoulizwa kama ratibu ngumu yenye mechi nyingi inaweza kuwafanya wachezaji wafanye mgomo, Rodri bla kupepesa alisema anadhani wanakaribia kufanya jambo hilo.
“Nadhani tunakaribia katika hilo, ni rahisi kuelewa, nafikiri ni jambo lililo wazi, nadhani kama utamuuliza mchezaji yeyote atasema hivyo hivyo, si mawazo ya Rodri au mtu mwingine mmoja, bali ni wazo la jumla kwa wachezaji wote,” alisema.
Rodri, 28, hata hivyo alisema hajui nini kitakachotokea lakini anachofahamu ni kwa wakati huu ni kwamba jambo hilo linawapa shida kwa sababu wao ndio wanaotaabika.
Mchezaji wa kimataifa anayeshiriki Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia la Klabu anaweza akafikisha mechi 85 au zaidi kwa msimu huu na Rodri tangu ajiunge na Man City mwaka 2019 amekuwa akicheza mechi zaidi ya 50 za klabu kwa msimu idadi ambayo anasema tayari ni kubwa.
