Eldoret, Kenya
Siku chache baada ya mwanariadha wa Uganda, Rebecca Cheptegei (pichani) kufariki kwa kuchomwa moto wa petroli, aliyekuwa rafiki yake wa kiume, Dickson Ndiema anayedaiwa kumfanyia ukatili huo naye amefariki dunia leo Jumanne.
Rebecca, 33 ambaye aliiwakilisha Uganda kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 hivi karibuni, alichomwa moto Septemba Mosi na kuungua zaidi ya asilimia 70 ya mwili wake kabla ya kufariki dunia siku nne baadaye.
Kifo cha Rebecca kilitokana na mzozo baina yake na Dickson chanzo kikidaiwa kuwa ni mgogoro baina ya wawili hao uliotokana na eneo la ardhi ambayo inadaiwa Rebecca aliinunua na kujenga nyumba.
Baada ya kifo cha Rebbeca ndugu zake na watu mbalimbali walisisitiza kutaka haki itendeke lakini kifo cha Dickson ambaye alikuwa mtuhumiwa mkuu kinazidi kuacha maswali kuhusu tukio hilo.
Wawili hao baada ya wote kuwa na majeraha ya moto walikimbizwa katika Hospitali ya Moi mjini Eldoret wakiwa na hali mbaya ingawa Rebecca ndiye aliyeungua sehemu kubwa ya mwili wake kumzidi Dickson.
Akizungumzia kifo cha Dickson, msemaji wa Hospitali ya Moi, Daniel Lang’at alisema kifo chake kilitokana na majeraha ya kuungua na moto.
Katika Michezo ya Olimpiki, Rebecca alishika nafasi ya 44 na baadhi ya makundi ya watetezi wa haki za wanawake wanahusisha kifo hicho na matukio ya unyanyasaji na unyonyaji wanaofanyiwa wanamichezo wanawake waliopata mafanikio.
Riadha Aliyemchoma moto mwanariadha naye afariki
Aliyemchoma moto mwanariadha naye afariki
Read also
