Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Azam imemtangaza Rachid Taoussi kutoka nchini Morocco kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo akichukua nafasi ya Youssouph Dabo aliyetimuliwa hivi karibuni.
Taarifa iliyopatikana leo Jumamosi kwenye vyanzo vya habari vya Azam FC ilieleza kuwa kocha huyo amekuja na benchi lake la ufundi kuanzia kocha msaidizi, Ouajou Driss.
Wasaidizi wengine wa kocha huyo ni kocha wa mapika, Rachid El Mekkaoui pamoja na kocha wa utimamu wa mwili, Badr Eddine.
“Tunayo furaha kumtangaza, Rachid Taoussi, kuwa kocha wetu mkuu mpya kwa mkataba wa mwaka mmoja,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ikiwa na picha ya kocha huyo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kocha Taoussi, amewahi kufanya kazi katika klabu za Waydad, CE Belouizdad, ES Setif na nyinginezo.
Dabo alitimuliwa Jumatatu iliyopita baada ya Azam kutolewa na APR ya Rwanda katika hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya timu hiyo kuwa na matarajio makubwa.
Azam chini ya Dabo ilitolewa na APR kwa jumla ya mabao 2-1, ikianza kwa ushindi wa bao 1-0 nyumbani kabla ya kulala kwa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano nchini Rwanda.
Soka Taoussi amrithi Dabo Azam FC
Taoussi amrithi Dabo Azam FC
Read also
