Na mwandishi wetu
Azam FC imetangaza kuachana na kocha wake, Youssouph Dabo ikiwa ni siku chache zimepita baada ya timu hiyo kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa ya klabu hiyo iliyopatikana leo Jumatatu imeeleza kuwa bodi ya wakurugenzi ya klabu pamoja na kocha huyo wamefikia makubaliano ya kutoendelea kufanya kazi pamoja.
Uamuzi huo unamfanya Dabo aondoke baada ya kuiongoza Azam kwa kipindi cha mwaka mmoja akijivunia kuifikisha nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu NBC lakini akashindwa kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa ya Azam ilieleza kuwa kocha huyo anaondoka na wasaidizi wake wote na imemshukuru kwa kipindi chote alichokuwa na timu hiyo na kumtakia kila la heri huko aendako na kumsifu kwa kufanya kazi kwa weledi na bila kukata tamaa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo baada ya Dabo kuondoka klabu imeanza mchakato wa kusaka kocha mpya ingawa kwa sasa timu hiyo itasimamiwa na jopo la makocha wa timu za vijana za Azam.
Baada ya Azam kutolewa katika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika ikikwama mbele ya APR ya Rwanda kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1, nafasi ya kocha Dabo ilianza kujadiliwa huku ikielezwa kwamba ajira yake ilikuwa njia panda.
Soka Dabo atimuliwa Azam
Dabo atimuliwa Azam
Read also
